"....tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.) 2 Wakorintho 6:2 “
Jana ni historia, kesho ni siri, leo ni zawadi kutoka kwa Mungu, ndiposa tunaiita present-zawadi.” —Bil Keane
Siku moja mwandishi aliyeitwa Leo Buscaglia alisimulia hadithi kuhusu mama yake na kile alichoita “chakula cha jioni cha familia na cha mateso.” Ulikuwa usiku ule wa kwanza baada ya baba yake kurudi nyumbani na akasema kwamba inaonekana kana kwamba itabidi afilisike kwa sababu mwenzi wake kibiashara alikuwa ametoroka na pesa za kampuni. Mama yake Buscaglia alienda kuuza vito ili anunue chakula kwa ajili ya karamu ya kukata na shoka.
Baadhi ya watu wa familia walimkemea kwa kuuza vito na kutumia pesa nyingi sana. Lakini yeye akawaambia, “ Wakati wa furaha ni sasa, wakati ambao tunaihitaji zaidi, na si wiki ijayo.”1 Ninapongeza hatua hiyo ya ujasiri na hekima ya mama huyu. Matumaini na furaha ni mambo mawili ambayo hayapaswi kuahirishwa kamwe.
Watu wengine huishi maisha yao wakingoja “kesho.” Husema, “Pengine kesho mambo yatakuwa bora zaidi,” au “Natumaini wakati wote kuna kesho,” au *“Natamani hii siku iishe na niione siku ya kesho.”* Wakati mtu anapoahirisha matumaini hadi kesho, hapati furaha ya leo, na hayo siyo maisha yaliyomfanya Yesu afe msalabani.
Yesu anataka tufurahie maisha yetu leo na kila siku. Amani, raha, furaha, kujiamini, ujasiri, afya, akili timamu, kibali, baraka, ndoa thabiti—haya yote ni mambo ambayo Mungu anapenda uanze kuyapokea leo. Kila wakati unaposema moyoni, Naona leo itakuwa siku ya hasara kabisa; pengine kesho itakuwa bora zaidi, unakosa mpango mzuri zaidi wa Mungu juu ya maisha yako. Ikiwa Mungu yuko pamoja nawe leo— na kweli yuko pamoja nawe; *Yuko nawe wakati wote—huna haja ya kusubiri wakati fulani ujao ndipo uanze kufurahi.
Unaweza kupokea maisha yaliyojaa furaha, ushindi na utele leo. Mtume Paulo alisema kwamba wakati kungali LEO, sharti tumsikie Mungu na tusiifanye mioyo yetu kuwa migumu dhidi ya ahadi zake (Waebrania 3:15).
Mungu anafanya kazi katika maisha yako leo, na anataka uamini leo na ufurahi leo! Zaburi 118:24, inasema, “Siku hii ndiyo aliyoifanya BWANA, Tutashangilia na kuifurahia” (imeongezwa msisitizo). Mungu aliifanya siku hii kwa sababu fulani. Kuna kitu maalum anachotaka kufanya. Je, uko tayari kukipokea? Natumai watu hufanya kile kinachoagizwa na kifungu hicho: Hushangilia na kuifurahia. Haijalishi hali ya hewa iko namna gani huko nje, jinsi wanavyohisi, yale yanayosemwa na watu, kuna vizuizi vinavyowakabili, au habari zinazotangazwa na vyombo vya habari—watu wenye matumaini husema, “Bwana ameiumba siku hii ya leo kwa sababu fulani— Nitashangilia na kufurahi.Nitakuwa na matarajio mazuri kwamba Mungu atatenda kitu kizuri maishani mwangu leo!”
Hebu niwasimulie hadithi inayonihusu mimi mwenyewe: Mnamo mwaka 2015 nilifikia kiwango cha kukata tamaa kuhusu hali yangu ya maisha. Nilidhani hakuna kitu kizuri kingetokea kwangu. Ingawa nilikuwa Mkristo, sikuwa ninapata ushindi maishani mwangu.
Siku moja nilipokuwa nimepanda gari kwenda kazini mwezi Februari mwaka huo, nilimlilia Mungu katika hali ya kushindwa nifanye nini na nafikiri kwa mara ya kwanza katika maisha yangu ya Ukristo niliwahi kupitia kitu kilichonifundisha imani haswa ni nini. Mungu alinihakikishia moyoni mwangu kwamba alikuwa anashughulikia hali yangu. Ingawa hakuna kitu kilichobadilika mara moja katika hali yangu, lakini baada ya hapo nilikuwa na amani kamili. Nilijaa matarajio mazuri kwamba kitu kizuri kilikuwa kinaenda kutokea siku hiyo! Nilikuwa na matumaini ya kweli! Sikujali Mungu alifanya nini, au hata alikifanya wakati gani, kwa sababu moyoni mwangu nilijua tayari imetendeka.
Ninaweza kusema wazi kwamba kuanzia wakati huo na kuendelea, mambo yalianza kubadilika katika maisha yangu. Hayakuwa kamili kwa vyovyote, lakini kidogo kidogo, siku hadi siku, mambo mazuri yalianza kutokea.
Ninajua unaweza kuwa unasema hivi: “Jimmy na je, ikiwa ninaamini kitu kizuri kitatokea leo na kisha kisitokee?” Kwanza kabisa, hebu niseme kwamba ninaamini kwa dhati ya kwamba kitu kizuri hutokea kila siku, lakini huenda tusikione. Pili, mambo mazuri yanayotokea huenda si yale tuliyotarajia haswa, lakini matumaini yalitupatia siku nzuri zaidi kushinda kile ambacho tungepata bila matumaini, kwa hiyo hilo pekee ni jambo zuri.
Na mwisho, nitasema kwamba sharti uamke tena kesho ukiwa na matumaini, ukiamini kwamba kitu kizuri kitatokea kwako siku hiyo. Haijalishi utafanya hivyo kwa siku ngapi, endelea kufanya hivyo, na utaona kwamba Mungu ni mwaminifu!!.
No comments:
Post a Comment