Nakumbuka siku moja nilipokea habari mbaya sana muda mfupi kabla kuaanza kongamano la siku tatu. Ilikuwa vigumu kuendelea, lakini nilijua sina budi kuendelea. Nilihisi Roho Mtakatifu akisema, “Nyanyua mguu wako na upige hatua kwenda mbele. Endelea kwenda Mbele!”
Kuendelea kwenda mbele hakukuondoa uchungu wote na hali ya kuvunjika moyo niliyohisi, lakini kulinizuia nisiweze kuzama katika kilindi cha kukata tamaa, na baada ya majuma machache, hali iliweza kutatuliwa. Moja ya dalili za ukomavu wa kiroho ni kuwa na nidhamu ya kutimiza ahadi zako, hata ikiwa unapitia wakati mgumu. Nilikuwa naumia, lakini nilihitaji kuendelea kuwahudumia wengine waliokuwa wanaumia, na nilifanya hivyo, Mungu aliniponya na kusuluhisha tatizo langu.
Hata hali iwe ngumu namna gani kumbuka tunapoumia, mambo huja na yakafikia mwisho. Majira ya kiangazi wakati wote huja baada ya majira ya baridi. Jua huwaka tena baada ya dhoruba. Jana kulitanda mawingu kutwa nzima, na hatimaye tukapata ngurumo za radi na mvuka kubwa, lakini leo anga ni la samawati na jua linawaka.
Nafikiri tunaweza kuona, hata katika mifumo ya kawaida ya hali ya hewa na mabadiliko ya majira, jinsi ambavyo mambo yalivyo mabaya yanavyotoa njia ya mambo mazuri. Ikiwa mawingu yametanda na kuna dhoruba maishani mwako leo, tazamia kwa hamu jua ambalo yamkini litang’aa kesho, siku itakayofuata au siku itakayofuatia ya pili.
Dhoruba haitadumu milele! Biblia inatoa mfano wa mwanamke mgonjwa (mwanamke aliyetoka damu) aliyepita katika mkutano kwa nyuma ili amfikie Yesu (Marko 5: 25-34; Luka 8:43-48). Hata ingawa mwanamke huyu alikuwa ameugua kwa miaka 12 na kumaliza pesa zake zote kwa waganga ambao walishindwa kumsaidia, alikataa kukaa tu, bila kufanya chochote akisubiri uchungu umwondokee. Aliamua kuruhusu matumaini yamhamasishe kupita katika kila tatizo.
Hakuna kitu ambacho kingemzuia asimfikie Yesu—si kundi la watu, si ugonjwa, si muda ule mrefu aliosubiri, si mashaka yake, si uchungu wake. Aliendelea kusema moyoni mwake Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona (Mathayo 9:21).
Aliendelea kwenda mbele, huku akiwa na matumaini na imani moyoni mwake. Huenda una kundi lako la watu unalopaswa kulipenya leo. Huenda ni kundi la mawazo mabaya. Huenda ni kundi la uchungu na maumivu ya zamani. Huenda ni kundi la watu waliokaribu yako wasiotaka kukusaidia. Huenda ni kundi la matatizo ya kifedha. Huenda ni kundi la uchungu mwilini mwako.
Lakini ukipita katikati ya mambo hayo yote na ukakataa kuruhusu mambo ya kuvunja moyo maishani yakukwamishe katika kilindi cha kuvunjika moyo na shida, utaupata ushindi wako.
Wafilipi 3:13-14 inasema: Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikie tuzo la thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.
(imeongezwa msisitizo) Napenda fungu hili la Maandiko.
Paulo alisema anayasahau yaliyopita—makosa na uchungu wa maisha yake ya awali—na alikuwa anakaza mwendo kwenda mbele kuifikia hatima yake. Unaweza kufanya vivyo hivyo. Unaweza kupita mambo hayo yote yanayoweza kukuzuia usiende mbele.
Leo unaweza kukataa kuwa na mtazamo wa kushindwa. Leo unaweza kukataa “kujifanya kifaurongo.” Unaweza kuchagua kuendelea kwenda mbele— unaweza kuchagua kukaza mwendo.
No comments:
Post a Comment