Friday, 6 July 2018

Hisia Usizoweza Kuzidhibiti

Watu wanaopitia msiba au pigo fulani mara nyingi  hupitia  hatua kadhaa katika hisia zao, kama kulia na kutoweza kujizuia. Hisia hizi zinaweza kutokea na kutoweka bila ya kutarajiwa. Dakika hii  mtu  yule  anaweza  kuwa  mzima  hana  neno.  Ghafla  anajikuta amekumbwa na kuwezwa na huzuni. 

Hata watu ambao kwa kawaida hawaonyeshi hisia zao kwa urahisi wanaweza kujikuta wanapatwa na hisia nyingi  mno wakati wa msiba au pigo. Mwanamume ambaye kwa kawaida halii anaweza kujikuta analia bila kujizuia mara kwa mara. Kwa ujumla,  watu huogopa hisia zao.  Na hata kuonyesha majonzi bila kujizuia huwatisha wengine.

Iwapo unapitia wakati mgumu sasa  hivi, ninakuhimiza “Usiogope” kwa sababu yale unayopitia sasa yatapita.  Ufahamu bora na msaada mwingi kutoka  kwa Roho Mtakatifu  utakupitisha hata nyakati ngumu zaidi. Watu wengine  hukataa  kulia  au kuonyesha hisia zozote, na hili si jambo jema. Hisia ambazo zimekaliwa ndani yetu zina nguvu nyingi na  zinahitaji kuachiliwa  na  kuondolewa.  Iwapo  hutoi na kuachilia hisia zako wakati wa msiba au pigo fulani, kama kifo cha mpendwa wako, unaweza kuanza kuliwa ndani yako na hisia hizo na mwishowe zinaweza kuharibu maisha yako kimwili, kiakili  na hata jinsi unavyohusika na mambo kihisia.

Kwa maana Mungu ametupatia machozi  pamoja  na uwezo wa kulia, basi inamaanisha  kuwa kutakuwa na nyakati katika maisha yetu ambapo tutahitaji kulia. Biblia inazungumza katika mahali tofauti kuhusu machozi.  Kwa mfano,  katika Zaburi 56:8, mtenzi anazungumzia chupa ambamo Mungu huyaweka machozi  yetu. Ufunuo 21:4 inazungumzia mbingu mpya na nchi mpya itakayoandaliwa siku moja  kwa ajili ya watu wa Mungu: “Mungu atayafuta machozi yao. 

Hakutakuwa na kifo tena, na wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu; maana mambo hayo yote ya awali yamekwisha toweka.” Kuna kulia kunakofaa na kulia kusikofaa. Kulia ili kuondoa hisia mbaya  ya  huzuni  ni bora, lakini  jihadhari usianze kujihurumia. Kusipoondolewa, basi kunaweza kuwa kama zimwi ambalo litakufanya uanze kujipinga mwenyewe, ambalo ni jambo lisilofaa.
Huruma ni karama ya Mungu ambayo ameweka ndani ya kila mmoja wetu ili tuweze kuwatambua na kuwageukia ili kuwasaidia wengine wanaoumia  mioyoni  mwao.  Lakini tunapojielekezea huruma hiyo, basi inaweza kutudhuru na kuleta ulemavu maishani mwetu.

Watu pia wanaweza kupatwa na uzoefu wa kujihurumia. Unaweza kufikiri  hii  ni  njia  ya  kujihudumia,  lakini  shetani  anaitumia kukuzuia usiendelee mbele katika maisha yako. Unahitaji kuwa mwangalifu usitumie machozi  yako kuwatawala wengine.
Wakati unapoumia moyoni, unawahitaji wengine wakuonyeshe upendo na ukarimu. Mara kwa mara, hata kama sisi ni watu wenye nguvu na wasiohitaji kuwategemea wengine, tutahitaji kusaidiwa na wengine kwa muda. Lakini tunafaa kukumbuka  kwamba ingawa kuna nyakati ambazo tunahitaji  usaidizi spesheli, watu  wengine  hawawezi kutatua  shida zetu.
Tunapowatazamia wengine tukitarajia watuondolee shida na uchungu wetu, basi tunakosea. Kwanza, kabisa, watu hawawezi kutupatia kila kitu tunachohitaji. Pili, kuwatarajia wengine wakutane na mahitaji yetu ya kibinafsi ni kuwapatia mzigo  mzito  kubeba. Hii huharibu mahusiano  yetu, hasa  ikiwa tabia hiyo  ya kuwategemea inaendelezwa  kwa muda mrefu. Inaeleweka wakati  mwanamke ambaye amempoteza mume wake anawageukia watoto wake ili wajaze pengo lililotokea maishani mwake.
Lakini ni vyema iwapo anafanya hivi kwa njia ya “kujitolea” kwa watoto wake zaidi  kwa maana  sasa  ana muda  na wakati wa kufanya hivyo. Lakini iwapo nia yake ni kuwalazimisha watoto hao wachukue jukumu la baba yao, wataichukia hali hiyo.
Kila mtu anafaa kuishi maisha yake, na hata kuwe na upendo kiasi gani kati ya watu wawili,  hakuna mtu anayetaka  kutawaliwa   kwa sababu za ubinafsi au kujipenda kwa mwenziye huyo. Iwapo  unapitia uchungu sasa  hivi,  ninakuhimiza umtegemee Mungu na umwache  afanye mabadiliko anayotaka katika mahusiano  yako.  Anajua  kuwa una mahitaji tofauti sasa.  Anajua kuna utupu  ambao unahitaji kujazwa.

Wakati  haya yanapotokea, Mungu atajaza pengo hilo iwapo tutamgojea na kutakataa kujaribu kutumia hisia zetu au kuwatawala wengine. Watu hawafanyi hivi  kimakusudi.  Yawezekana ni kwa sababu tunaumia moyoni  au tunatafuta kitu chochote  ambacho  kinaweza kuondoa uchungu wetu. Lakini Mungu hafanyi uponyaji kwa kumwondolea mmoja mzigo na kumwekea mwingine mzigo ule. Mapigo na misiba hutuacha katika hali ya unyonge, na shetani atajaribu kutuvamia wakati tumechoka kabisa. 
Shetani haoni haya kutuvamia hata  wakati  tumeanguka  chini na kushindwa. Yeye huona nyakati  hizo tunapokuwa  wapweke  na wenye  uchungu kama nafasi bora ya kutufunga na kutuweka katika majonzi. Kutembea kwa  usawa  kutamfungia shetani mlango asiingie. Baada ya miaka mingi, nimegundua kuwa ni lazima tujifunze kupitia mambo  mengine kwa siri. Hii haimaanishi  kuwa hatuwahitaji  watu wengine, kwa sababu tunawahitaji.  Watu wengine hutumiwa na Mungu kutuletea faraja tunapokuwa tunaumia moyoni.  Hata hivyo, iwapo “kuwahitaji” watu maishani mwetu kutapita kiasi kilicho  sawa,  basi huenda  tukamzuia Mungu kufanya kazi katika maisha yetu.

Moja  ya faida  ya kukosa mtu wa  kugeukia isipokuwa  Mungu ni kwamba tunapata nafasi ya kuimarisha mizizi yetu “ndani yake”.   Yeye ndiye mwamba, msingi ulio imara ambao hautikisiki. Haijalishi kama mengine yanatikisika.  Yeye yu imara. Iwapo  unaomboleza au u mpweke kutokana na pigo au mkasa fulani katika maisha  yako, geuza tukio hilo  liwe  nafasi  nzuri ya kuingia katika uhusiano wa ndani kati yako na Mungu Baba, Mungu Mwana na Roho Mtakatifu.

Kumbuka:  Shetani anataka kutumia nyakati kama hizo kukuangamiza, lakini kile ambacho amepanga kikudhuru, kitaishia kuwa  baraka kwako,  unapoendelea  kumtegemea. (Mwanzo 50: 20; Warumi 8:28)
Mtumishi Jimmy J.

No comments:

Post a Comment