Sunday, 2 September 2018

MAGEUZI YA UPENDO

Mageuzi.   Neno lenyewe linaibua  tumaini, linawasha  hamu na kuvutia uaminifu  kama  neno  ambalo halijawahi kupatikana kwenye msamiati wa  binadamu. Katika historia,  wazo  la maguezi limemimina  mafuta kwenye moto na kusisimua ujasiri kwa waliovunjika moyo.

Mageuzi yamewakusanya pamoja  wale wanaotafuta  sababu kubwa  kuliko  wao  wenyewe na  yamewapa wanawake na wanaume waliokosa  mwelekeo hapo  awali, sababu ya kujitoa mhanga.
Wamewazaa  viongozi mashuhuri  na kuwalea wafuasi mashuhuri, wameubadili kabisa ulimwengu. Mageuzi ni  jambo la ghafla, kubwa  na lililo  tofauti kabisa na jinsi  mambo yalivyo kama  kawaida.  

Mageuzi huchochewa  na mtu mmoja au kundi  dogo sana la watu wasiokubali  kuendelea  kuishi kama  walivyokuwa  siku zilizopita. 

Wanaamini  kuwa  lazima  jambo fulani lifanyiwe mabadiliko  na  huendelea  kuimarisha  mawazo yao  hadi pale msingi wao  unapoanzia  na hilo hatimaye huleta mabadiliko kwa njia kubwa.
Nimeishi  kwa muda wa miaka ishirini na kadhaa  ninapoandika kitabu hiki, na ninadhani kwamba nikiwa peke yangu nimejua mambo machache  tu. Ninaweza  kusema nimeishi  kwa  muda mrefu  kiasi, kuweza  kujaribu njia mbali mbali za  kupata  furaha  na  nimegundua jambo  hilo kwa  kufanya  chaguo  kuhusu kile kinachofanya  kazi na  kisichofanya  kazi. 

Uchoyo  haufanyi  maisha  kuendelea  kama yalivyonuiwa na hivyo basi haupo  kwenye mpango wa  Mungu kwa  binadamu. Ninaamini ninaweza  kuthibitisha  katika  kitabu hiki  kwamba  uchoyo kwa  kweli  ndilo  tatizo kuu  linalotukabili  hivi leo ulimwenguni na  kwamba  juhudi  kubwa  za  kuuangamiza  uovu huu ndilo litakalokuwa  jibu letu. Twahitaji  kutangaza  vita  dhidi ya uchoyo. Twahitaji Mageuzi ya Upendo.
Upendo lazima  uwe zaidi ya  mtazamo  au  neno, lazima utekelezwe kwa vitendo. Lazima uonekane na watu wauhisi. Mungu ni  Upendo! Upendo  umekuweko na kila mara utakuwa  wazo  lake Mola.  Alikuja ili  kutupenda, kutufunza jinsi  ya  kumpenda  Mola,  na kutufunza jinsi ya kujipenda na kuwapenda watu wengine.

Tunapofanya hivi  maisha yatakuwa  mema; tusipofanya hivi hakuna kinachofanyika  kwa  njia nzuri. Upendo ndilo  jibu la uchoyo kwa  sababu upendo hutoa,  ilhali uchoyo huchukua.  Lazima tukombolewe kutoka  kwa  nafsi zetu,  na  Yesu alikuja kwa  kusudi hili  kama  tunavyoona  katika 2 Wakorintho 5:15 “ ?Tena alikufa kwa ajili ya  wote,  ili walio  hai  wasiwe hai  tena  kwa  ajili ya  nafsi zao wenyewe, bali kwa  ajili yake Yeye aliyekufa akafufuka kwa  ajili yao.”

Nimekataa  kusimama kutazama  bila kufanya lolote ilhali ulimwengu unazidi kudidimia. Huenda nisiweze kutatua matatizo yote  ninayoyaona,  lakini nitafanya  lile  niwezalo.  Ombi langu  ni kwamba uungane nami katika kuchukua msimamo dhidi ya ukiukaji wa  haki na kuwa  tayari kuleta mabadiliko katika  njia ya  maisha unayochagua.  Maisha  si kuhusu kile ambacho  wengine wanaweza kutufanyia sisi, bali ni kuhusu kile tunachoweza  kuwafanyia wengine.

Ninachagua huruma na kusalimisha misamaha yangu. Ninapinga maovu na kujitolea kufanya matendo ya Upendo wa Mungu. Ninakataa kutofanya lolote. Huu ndio uamuzi wangu. MIMI NI MAGEUZI YA UPENDO.

Ninaomba kwamba  maneno  haya pia yatakuwa wito wako, mtindo mpya  utakaouzingatia maishani. Usisubiri  kuona kile mtu mwingine anachochagua  kufanya  na  usisubiri  kuona  ikiwa vuguvugu limeanza  kuwa  maarufu. Hili  ni jambo ambalo  lazima wewe mwenyewe ufanye uamuzi, kujitolea ambako  wewe peke yako lazima uchague kukufanya.

Hebu  jiulize, “Je, nitaendelea  kuwa sehemu  ya  tatizo  hili  au nitakuwa  sehemu  ya  jibu?”  Nimeamua kuwa  sehemu  ya  jibu. Upendo ndio utakaokuwa  mwito wa  maisha yangu.

Na je, wewe?  Utachochea  matatizo yaliyoko ulimwenguni? Utayapuuza  au kujifanya  kuwa  huyaoni? Au utajiunga  na Mageuzi ya Upendo?

Karibu ujipatie Nakala ya kitabu hiki.

No comments:

Post a Comment