Ninachagua huruma na kusalimisha misamaha yangu. Ninapinga maovu na kujitolea kufanya matendo ya Upendo wa Mungu. Ninakataa kutofanya lolote. Huu ndio uamuzi wangu. MIMI NI MAGEUZI YA UPENDO.- Imani yetu.
Mageuzi ni jambo la ghafla, kubwa na lililo tofauti kabisa na jinsi mambo yalivyo kama kawaida. Mageuzi huchochewa na mtu mmoja au kundi dogo sana la watu wasiokubali kuendelea kuishi kama walivyokuwa siku zilizopita. Wanaamini kuwa lazima jambo fulani lifanyiwe mabadiliko na huendelea kuimarisha mawazo yao hadi pale msingi wao unapoanzia na hilo hatimaye huleta mabadiliko kwa njia kubwa.
Mageuzi yamewakusanya pamoja wale wanaotafuta sababu kubwa kuliko wao wenyewe na yamewapa wanawake na wanaume waliokosa mwelekeo hapo awali, sababu ya kujitoa mhanga. Wamewazaa viongozi mashuhuri na kuwalea wafuasi mashuhuri, wameubadili kabisa ulimwengu.
Thomas Jefferson alisema “ Kila kizazi chahitaji mageuzi mapya ” na ninaamini huu ndio wakati wa mageuzi yajayo ya Ulimwengu, mageuzi makuu sana kwa watu wote. Hatuhitaji mageuzi sawa na yale yaliyoharibu nchi ya historia ya ulimwengu katika vizazi vilivyotutangulia, hatuhitaji mageuzi yanayozingatia siasa, chumi, au teknolojia. Twahitaji Mageuzi ya Upendo.
Twahitaji kupindua hali ya uchoyo, hali ya kuishi katika ubinafsi maishani mwetu. Hakuna kitakachobadilika katika ulimwengu wetu hadi pale kila mmoja wetu atakapokuwa radhi kubadilika. Mara nyingi huwa tunatamani ulimwengu ubadilike bila ya kukoma kutambua kwamba hali ilivyo ulimwenguni inatokana na njia tunazoishi katika maisha ya ubinafsi na chaguo tunalofanya kila siku. Ikiwa kila mmoja hapa duniani anafahamu jinsi ya kupokea na kuonyesha upendo, dunia yetu ingelikuwa mahali tofauti kabisa pa kuishi. Nafikiri sote twafahamu kuwa kuna jambo lililo kasoro katika jamii na kwamba lahitaji kutatuliwa. Lakini hakuna mtu anayefahamu kinachopaswa kufanywa au jinsi ya kuanza kufanya mabadiliko. Jibu letu kwa ulimwengu usioweza kuthibitika ni kulalamika na kufikiri, kuna mtu anayepaswa kufanya jambo fulani.
Tunafikiri na kusema kuwa pengine Mungu au serikali au mtu mwingine yeyote aliye kwenye mamlaka anahitajika kufanya kitendo. Lakini ukweli ni kwamba kila mmoja wetu anahitajika kufanya jambo fulani. Lazima tujifunze kuishi maisha yenye mwelekeo tofauti kabisa na tulivyo sasa. Lazima tuwe radhi kujifunza, kubadilika na kukubali kwamba sisi ni sehemu ya tatizo lililoko. Hatuwezi kutatua kile tusichoelewa, kwa hiyo hitaji letu la kwanza ni kutafuta chanzo cha tatizo lililoko.
Ni kwanini watu wengi hawana furaha? Ni kwanini ghasia zimeongezeka sana katika familia, maeneo jirani, miji na mataifa? Ni kwanini watu wana hasira nyingi? Unaweza kufikiri kuwa mambo haya yanatendeka kwa sababu ya dhambi. Unaweza kusema “Watu ni wenye dhambi. Hilo ndilo tatizo.” Nakubali usemi huo, lakini ningependa kulikabili tatizo hili kwa mtazamo wa vitendo tunavyokumbana navyo kila siku. Ninaamini kikamilifu kuwa chanzo cha maswala haya na mengine ni Uchoyo.
Uchoyo kwa kweli ndio chanzo cha dhambi. Ni mtu kusema, “Ninataka kile ninachokitaka na nitafanya kile ninachohitaji kufanya nipate nikitakacho.” Dhambi huweko wakati mtu anapofanya kinyume na mapenzi ya Mungu na njia Zake. Tunaishi “nyuma” kinyume kabisa na tunavyopaswa kuishi. Tunaishi kwa kujijali sisi wenyewe ilhali hatupati kile kinachoturidhisha. Twapaswa kuishi kwa kuwajali wengine na tujifunze siri ya ajabu kwamba kile tunachotoa huturudia kikiwa kimeongezeka zaidi ya maradufu.
Ninapenda sana jinsi daktari mmoja mashuhuri kwa jina Luka alivyosema. “Yatoe maisha yako, nawe utaregeshewa maisha hayo, lakini sio kuregeshewa maisha tu, utaregeshewa pamoja na bakshishi na baraka. Kutoa wala sio kupokea ndio njia. Ukarimu hulipwa ukarimu.” (LK 6:38 The Message).
Katika jamii nyingi, urithi, umiliki na uthibiti ndilo lengo kuu la watu wengi. Kila mmoja anataka kuwa wa kwanza kumiliki, hii ikionyesha moja kwa moja kwamba watu wengi watakasirika kwani ni mmoja tu atakayekuwa wa kwanza kila wakati katika sehemu yoyote. Ni mtu mmoja tu anayeweza kuwa wa kwanza katika mashindano ya mbio duniani, ni mtu mmoja tu anayeweza kuwa rais wa kampuni au mchezaji sinema bora. Ni mtu mmoja tu anayeweza kuwa mwandishi bora wa kitabu au mchoraji bora duniani. Ingawa ninaamini kuwa tunapaswa kuwa na lengo na kujitahidi, siamini kuwa tunapaswa kutaka kila kitu kiwe chetu na kutowajali watu wengine..
Nimekataa kusimama kutazama bila kufanya lolote ilhali ulimwengu unazidi kudidimia. Huenda nisiweze kutatua matatizo yote ninayoyaona, lakini nitafanya lile niwezalo. Ombi langu ni kwamba uungane nami katika kuchukua msimamo dhidi ya ukiukaji wa haki na kuwa tayari kuleta mabadiliko katika njia ya maisha unayochagua. Maisha si kuhusu kile ambacho wengine wanaweza kutufanyia sisi, bali ni kuhusu kile tunachoweza kuwafanyia wengine.
Kila vuguvugu lahitaji maudhui au wito wa kuendeleza. Sisi katika huduma ya Mageuzi ya Upendo tumeweka nadhiri kupitia maombi tuliyojitolea kuzingatia maishani. Je, utaungana nasi?
Pata Nakala yako ya Mageuzi ya Upendo tujifunze pamoja.
Jimmy J.
Mwana Mageuzi
Jimmy J.
Mwana Mageuzi
No comments:
Post a Comment