Wednesday, 25 October 2017

QUR'AN YAKIRI YESU NI MUNGU


Utangulizi 

Yesu Kristo ni mtu mwenye ushawishi mkubwa sana duniani kuliko mtu yeyote tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Watu wengi wanamtambua kama Mungu, hasa Wakristo. Vile vile, wako wengine wengi ambao hawamtambui kama Mungu, hasa Waislamu. Tunaweza kubishania suala la Yesu Kristo kuwa Mungu au kutokuwa Mungu hadi siku ya kiama huku kila mtu akishikilia msimamo wake. Kila upande unajaribu kutoa hoja za kutetea msimamo wake. Pamoja na kutofautiana huko, lakini jambo moja ni dhahiri. Ama wanaosema Yesu Kristo ni Mungu wako sahihi au wanaosema Yesu Kristo si Mungu wako sahihi. Basi! Haiwezekani kamwe pande zote mbili zikawa sahihi! 
Biblia inatamka wazi kwamba Yesu Kristo ni Mungu. Je, ni kweli kwamba Quran haimtambui Isa/Yesu kama Mungu? Katika kitabu hiki tutafahamu jibu la swali hili. Huenda ni jibu ambalo hulitarajii kabisa na litakufanya uwe na mtazamo mpya kabisa ambao hujawahi kuwa nao! Hatimaye, itakuwa ni juu yako kukubali maandiko au kuyakataa! Kuamini jambo ni ulichukulia kuwa ni kweli wakati hatulioni. Hata hivyo, katika kuliamini jambo hilo, huwa tunakuwa makini kutafuta ushahidi unaothibitisha kuwa tulichokiamini ni sawa au la, ili yamkini tusijekuwa tumeamini kisicho sahihi au tumeamini isivyo sahihi. 
Neno Kuhusu Kuamini 
Ni mara nyingi tumeamini maneno tuliyoambiwa na watu mbalimbali. Maneno hayo yaweza kuwa ni ahadi za mdomo, matangazo ya biashara redioni, mahubiri kwenye nyumba za ibada, n.k. Japokuwa imani si jambo baya, lakini linaweza kuwa na hatari moja kubwa. Hatari hiyo ni kwamba, watu wengine wanaweza kutumia kwa faida zao binafsi ile nia yetu nzuri ya kuwaamini. Kwa hiyo, ni jambo la muhimu sana tena sana kutafuta ushahidi au kuyapima tena na tena yale tunayoyaamini ili tusije kupata hasara mwisho wa safari 
ambapo hatutakuwa tena na nafasi ya kurekebisha mambo hata kama tutataka kufanya hivyo. Vivyo hivyo, kwa upande wa dini ni muhimu sana kujua kile ambacho Mungu anatuagiza – tuwe Waislamu au Wakristo. Kwanza ni lazima sisi wenyewe tuwe na ufahamu kuhusu maneno ya Mungu. Tukiwa nao huo ufahamu wa maneno au maagizo ya Mungu, tutaweza kupima yale yote ambayo watu mbalimbali watatujia na kutuambia, ‘Mungu anasema hivi na hivi.’ Vinginevyo tunaweza kujikuta tumeingia kwenye mtego wa kushabikia dini badala ya kuishabikia ‘kweli’. Kama tutakuwa hatujui Mungu anasema nini, watu wasio na nia njema watatuhubiria mafundisho yasiyo sahihi na sisi tutawaamini kwa moyo wote tena kwa nia njema kabisa, kwa vile tutakuwa tukidhani 
kuwa hivyo ndivyo Mungu anavyosema. Waislamu ni watu wenye bidii sana katika kumtafuta na kumtumikia Mungu. Ni jambo la pekee sana kwa mtu kwenda kwenye nyumba ya ibada mara tano kila siku, tena kuanzia alfajiri sana wakati mwili bado unakulazimisha kulala usingizi. Ni mtu gani atakayekubali kufanya jambo kama hilo isipokuwa yule mwenye nia ya kweli ya kumtafuta Mungu? 
Tumesikia mara kadhaa watu wakijitoa muhanga maisha yao kwa ajili ya Mungu. Japo siafiki jambo hilo, lakini tukiachana na suala la kwamba ni sahihi au si sahihi kufanya hivyo, halafu tukaichunguza tu ile nia yenyewe ya kufanya hivyo, nakiri kabisa kutoka moyoni kuwa, kitendo hicho kinadhihirisha moyo mkuu na nia ya kweli ya kumtafuta Mungu. Swali linabaki tu kuwa, “Je, hivyo ndivyo kweli alivyoagiza Mungu?” Maana ni vigumu sana kuamini kuwa baba mwenye watoto kumi atafurahia na kumpongeza mwanawe mmoja atakayemjia na kusema, ‘Baba nimeua ndugu zangu wawili kama ulivyoagiza.’ Au kwamba baba mwenye wanawe atatoa amri kuwa, yule atakayeua ndugu zake nitampenda zaidi! Hata hivyo, ni lazima kutambua ukweli kwamba, tukiamini jambo lisilo sawa, hata kama nia yetu ni njema kabisa, tutaishia pabaya tu! Siku hiyo 
hatutamwambia Mungu, ‘Mimi nilidhani hivyo ndivyo ulivyosema; maana nilifundishwa hivyo.’ Kwani mtu akinywa sumu inayofanana kabisa na maji itakuwaje? Je, atakayekufa ni yule tu aliyekuwa na nia ya kujiua? Si hata yule ambaye kwa nia njema alitaka kukata kiu akidhani hayo ni maji naye atakufa? Je, nia yake njema ya kukata kiu itamwokoa na mauti? La hasha! Aliamini, lakini imani yake ilikuwa katika jambo lisilo sahihi – mauti haitamwacha hata kidogo! Vivyo hivyo, ni lazima tutambue kuwa kuna 0watu wanaosimama mbele ya wengine na kusema kuwa wanaleta ujumbe wa Mungu, lakini ukweli ni kuwa ujumbe wanaoleta si wa Mungu hata kidogo. Watu wa aina hii wapo katika dini za aina zote. Kuna watu wanaotumia dini na Jina la Mungu kutafuta umaarufu au utajiri kwa kupitia kwenye hali ya kutoelewa 
ya watu wengi au kupitia kwa wale wasiotaka kutafuta ukweli wa mambo yale wanayoambiwa. Wengine wanatafuta tu kushiba, yaani wameshindwa kutafuta fedha kwa njia zingine, hivyo wanatumia nyumba za ibada kama genge la kupatia mahitaji yao ya kila siku. Watu wa aina hii ni lazima maneno yao yatachanganywa na uongo mwingi. Ni mara ngapi tumesikia wale wanaojiita kuwa wachungaji lakini wamekamatwa na dawa za kulevya? Nirudie tena kusema kwamba wadanganyifu wanaotumia jina la Mungu kujinufaisha ni wengi na wapo katika dini zote. Ni mtu yule tu anayejua Mungu anasema nini ndiye atakayeweza kupambanua kati ya mafundisho ya kweli na mafundisho ya uongo. Mtu asiyejua maandiko yanasema nini ni lazima atadanganywa tu! Je, wewe una uhakika kuwa yale unayohubiriwa yote ni maagizo ya Mungu? 

Mambo Yanayopingana 
Tunapokuwa shuleni katika somo la lugha, huwa tunafundishwa kuhusu kinyume cha maneno. Walimu hutufundisha kuwa kinyume cha ‘simama’ ni ‘kaa’; kinyume cha ‘nzuri’ ni ‘mbaya’ n.k. Lakini kuna aina kuu mbili za kinyume, yaani kinyume kisicho kamili na kinyume kamili. KINYUME KISICHO KAMILI Kinyume kisicho kamili maana yake ni kwamba unakuwa na Neno A ambalo kinyume chake ni Neno B. Lakini hicho kinyume si kinyume ‘pekee’ cha hilo Neno A. Kwa mfano, tukiulizwa tutaje kinyume cha neno ‘mrefu’ ni rahisi tu kwa wengi kusema kuwa kinyume chake ni neno ‘mfupi’. Hata hivyo, ukichunguza maana ya neno ‘mfupi’, utakutana na ugumu wa namna fulani utakaokulazimisha kufikiria upya jibu hilo. Ni vivyo hivyo kusema kuwa kinyume cha neno ‘mkubwa’ ni ‘mdogo’. Hebu tuchunguze mfano ufuatao wa vitu vitatu, tembo, ng’ombe na kondoo. 
Ukichunguza kwa mfanohuu wazi utaona kuwa: 
(a) Tembo ni mkubwa kuliko ng’ombe. 
(b) Ng’ombe ni mdogo kuliko tembo. 
(c) Ng’ombe ni mkubwa kuliko kondoo. 
(d) Kondoo ni mdogo kuliko ng’ombe. 
Sasa, kama kinyume cha mkubwa ni mdogo, iweje basi ng’ombe awe ni mdogo na wakati huohuo ni mkubwa? Kumbe hii ina maana kuwa upande mmoja ukiwa na neno ‘mkubwa’ kinyume chake si lazima kiwe ni ‘mdogo’. Badala yake, kati ya maneno haya, unaweza kuwa na viwango mbalimbali. Ndiyo maana tunaweza kusema kondoo ni mkubwa, ng’ombe ni mkubwa zaidi na tembo ni mkubwa zaidi sana. Pia, tunaweza kusema, tembo ni mdogo, ng’ombe ni mdogo zaidi na kondoo ni mdogo zaidi sana. 
Maneno mengine yenye tabia hii ni pamoja na mrefu na mfupi, nzuri na mbaya, ghali na nafuu, mbali na karibu, n.k. Kutokana na ukweli huu, tukija upande wa mitazamo tutagundua kuwa, watu wawili wanaweza kutofautiana katika jambo na bado wote wakawa wako sahihi kabisa endapo jambo lenyewe linahusu kinyume kisicho kamili. Mathalani, mtu atakayesema kuwa Marko ni mfupi, atakuwa sahihi kabisa kwa kuwa kuna kigezo cha kweli kinachoruhusu mtazamo huo; maana inategemea anamlinganisha na nani. Na yule atakayesema kuwa Marko huyohuyo ni mrefu naye atakuwa sahihi kwa kuwa atakuwa anamlinganisha na mtu mwingine. Nguo iliyo ghali kwangu (kwa vile kipato changu ni kidogo), itakuwa bei chee kwako (kwa vile kipato chako ni kikubwa). Kwa hiyo, mimi nikisema ni bei ghali, niko sahihi na wewe ukisema ni bei chee, uko sahihi. KINYUME KAMILI Kwa upande wa pili, kinyume kamili au halisi maana yake ni kuwa, kama Neno A liko katika kundi hili, ni lazima; narudia tena, ni lazima kinyume chake kiwe ni Neno B. Si vinginevyo! Kwa mfano kinyume cha neno ‘mfu’ ni neno ‘hai’. Basi! Kama mtu hajafa, basi ni lazima atakuwa hai tu! Na kama atakuwa si hai, ni lazima awe amekufa! 
Hakuna viwango mbalimbali katika aina hii ya kinyume. Yaani, huwezi kuwa hai, hai zaidi, hai zaidi sana; au ukawa na mfu, mfu zaidi, mfu zaidi sana. Haiwezekani! Ama mtu amekufa au yuko hai. Basi! Sasa, itakuwaje pale watu wawili watakapoanza kubishana kuhusu kuku? Mmoja akasema, “E bwana ee, huyu kuku amekufa.” Mwingine akasema, “Hapana. Huyu kuku yuko hai.” Hapo utajua wazi kuwa ni mmoja tu kati yao ndiye aliye sahihi. Si wote. Hapana! Hapana! Lakini kama wakibishana kwa mmoja kusema kuwa kuku huyo ni mzuri na mwingine akasema ni mbaya, wote watakuwa sahihi. TOFAUTI YA UISLAMU NA UKRISTO Yapo mambo kadhaa ambayo kwayo Waislamu na Wakristo wanakinzana au kupingana. Katika mambo yale yanayohusu kinyume kisicho kamili kama tulivyoona hapo juu, wanaweza kukinzana na bado wote wakawa sahihi. Hivyo, yapo mambo ambayo yanahusu aina ya pili ya kinyume, yaani kinyume kamili. Haiwezekani hata kidogo wote wakawa sahihi. Ama Waislamu watakuwa sahihi au Wakristo watakuwa sahihi katika mambo ya aina hiyo. Basi! Mambo yanayohusu kinyume kamili yanaweza kuwa mengi, lakini ifuatayo ni orodha fupi inayohusu baadhi yake: 
(a) Waislamu wanasema Isa/Yesu hakufa; Wakristo wanasema alikufa. 
(b) Waislamu wanasema Isa/Yesu si Mungu; Wakristo wanasema ni Mungu. 
(c) Waislamu wanasema majini wazuri wapo; Wakristo wanasema majini wazuri hakuna. 
(d) Waislamu wanasema Ibrahimu aliambiwa amtoe kafara Ishmael; Wakristo wanasema Ibrahimu aliambiwa amtoe Isaka. 
(e) Waislamu wanasema ndoa si lazima iwe ya mke mmoja; Wakristo wanasema ndoa ni lazima iwe ya mke mmoja. 
(f) Waislamu wanasema matendo mema ndiyo msingi wa kutuingiza mbinguni (peponi) na kutuepusha na jehanamu; Wakristo wanasema matendo mema kamwe si msingi wa kutuingiza mbinguni na kutuepusha na jehanamu. 
Haya ni baadhi ya mambo ya msingi kabisa katika maisha ya imani. Swali kuu la kujiuliza ni kuwa, “Inawezekanaje pande zote mbili zikawa sahihi katika mambo haya?” Jibu ni wazi tu, Haiwezekani! Upande mmoja tu ndio utakaokuwa sahihi. Ama ni Uislamu au ni Ukristo! Kwa mfano, haiwezekani hata kidogo ikawa kwamba Isa/Yesu alikufa na wakati huo huo hakufa. Jibu ni moja tu. Ama alikufa au hakufa. Ama Uislamu uko sahihi au Ukristo uko sahihi. Basi! Si pande zote mbili. Hapana! 

Vilevile, haiwezekani Waislamu wakasema Ibrahimu hakuambiwa amtoe Isaka kuwa kafara; na Wakristo wakasema Ibrahimu hakuambiwa amtoe Ishmaeli kafara; halafu wote wakawa sahihi. Hapa ni upande mmoja tu utakuwa sahihi. Si pande zote! Ni juu yako wewe na mimi kuitafuta kweli. Haya si mambo yanayohusu utajiri na heshima ambayo ni mambo ya hapa hapa duniani. Maana utajiri au heshima ukiupoteza waweza kuupata tena. Lakini, mambo haya yanahusu uzima wa milele; au mauti ya milele. Ndiyo yanayoamua mimi na wewe tutakuwa mbinguni milele au jehanamu milele. Milele! Basi, hata ukiamua kuamini, ni vema ukawa na majibu ya kujiridhisha wewe mwenyewe kuhusu masuala kama haya. Usiishie tu kusema, ‘Mimi naamini tu.’ Ukiulizwa, au hata ukijiuliza mwenyewe kwa nini unaamini hivyo, kisha ukasema, ‘Naamini tu’, ni wazi hapo kuna hatari ya kuangamia milele – uwe Muislamu, Mkristo au imani nyingine yoyote. Kwa upande wa Wakristo, wao wanaambiwa na maandiko kuwa, “Msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.” (1Yohana 4:1). 

Hapa haimaanishi kujaribu mambo yanayosemwa na wasio Wakristo. Hapana! Ni pamoja na yale yanayosemwa na wahubiri wakubwa na maarufu wa Kikristo. Ukishamsikiliza ni lazima upime na kuchunguza yale aliyokuhubiria kama ni ya Mungu, bila kujali mhubiri huyo ni maarufu kiasi gani. Maadamu yeye ni mwanadamu, bado anaweza kuingiza na ya kwake. Usipopima, uko kwenye hatari ya kupotoshwa. Sasa unapimaje roho? Unasoma maandiko ya Mungu wewe mwenyewe, ili atakapokuja mtu anakuambia Mungu anasema hivi na hivi, uweze kujua kuwa ni kweli au si kweli. Usipojua maandiko, hutajua hata kidogo pale mtu atakapokuhubiria, kumbe anahubiri mambo kutoka tu moyoni mwake. 
Imani, kimsingi ni kukubali kwamba kitu au jambo fulani lipo wakati hatulioni. Kwa mfano, kwa kuwa tunakubali kuwa Mungu yupo, na kwa vile hatumuoni, hiyo ni imani; tunaamini au tuna imani juu ya kuwapo kwa Mungu. Huwezi kusema kuwa unaamini kuwa una kichwa, maana hicho unakiona! 
Thamani ya Imani Sahihi 

Imani juu ya Mungu ni kitu chenye thamani kuliko kitu kingine chochote maishani. Hii ni kwa sababu, maisha ni ya muda lakini Mungu ni wa milele na milele na milele! Hivyo, imani, ama itanipeleka mbinguni milele au motoni milele. Na tukishatoka katika dunia hii, hatutapata nafasi tena ya kurekebisha mambo! Kwa hiyo, ni muhimu sana kufamu vyema kile ambacho mtu anakiamini ili tusije tukaishi kwa hasara na kuishia kujuta milele. Ni vema basi kila mmoja wetu akajiuliza swali lifuatalo: Je, kila ninachokiamini ndicho anachosema Mungu au vingine ni maagizo ya wanadamu? Kwa njia ya imani tunaponya roho zetu, yaani uhai wetu; au tunazipoteza milele. Imani sahihi ni jambo ambalo thamani yake inapita kila utajiri unaoweza kuufikiria. Wakati wa majira ya Krismasi ya mwaka 2007, shekhe mmoja maarufu jijini Dar es Salaam katika kipindi chake kimoja cha televisheni alisema kuwa, Isa/Yesu si wa Wakristo peke yao, bali ni wa Waislamu pia. Mimi hilo neno lilinipa changamoto kubwa. Katika kufuatilia, nikagundua ukweli mwingi sana kuhusu maneno ya shekhe huyo kuliko ambavyo nilitarajia. Kumbe Quran inamtaja Yesu Kristo kwa uzito sana, pengine kuliko ambavyo wengi tunafahamu; kuliko ambavyo tumeelezwa au tunaweza kuamini! Sasa nikabaki najiuliza: Tunaachania wapi? Mivutano inatoka wapi? Je, ni wangapi wanaufahamu ukweli wote? Basi katika kijitabu hiki kidogo, nitatumia rejea za lugha ya Kiingereza ambazo nitazitafsiri kwa Kiswahili. Rejea hizo zinatoka katika (ninanukuu Kitabu hicho kilivyoandikwa): “The Quran, An English Translation of the Meaning of the Quran; Checked and Revised by Mahmud Y. Zayid; Assisted by a Committee of Muslim Scholars; Approved by the Supreme Sunni and Shii Councils of the Republic of Lebanon, Dar Al-Choura; First Edition 1980.” (Mwisho wa kunukuu). 
Yaani, “Quran, Tafsiri ya Kiingereza ya Maana ya Quran; Iliyochekiwa na kusahihishwa na Mahmud Y. Zayid; Akisaidiwa na Kamati ya Wasomi wa Kiislamu; Imeidhinishwa na Mabaraza Makuu ya Kisuni na Kishia ya Jamhuri ya Lebanoni, Dar Al-Choura; Toleo la Kwanza 1980.” Kwa hiyo, marejeo haya yanatokana na Kitabu cha Quran ambacho kimehakikiwa na wanazuoni waliobobea katika kazi waliyoifanya. 

Quran Isemavyo Kuhusu Torati 
na Injili 
Kabla ya kuletwa kwa Quran, kulikuwa na vitabu vingine vya Mungu walivyoletewa wanadamu. Lakini kabla ya yote, hebu tuone Allah anasemaje ndani ya Quran yenyewe: Allah! There is no god but Him, the Living, the Ever-existent One. He has revealed to you the Book with the truth confirming what preceded it; and He has already revealed the Torah and the Gospel for the guidance of men, and for the distinction between right and wrong. 
Yaani: Allah! Hakuna mungu isipokuwa Yeye, aliye hai na wa milele. Amewafunulia kitabu chenye ukweli kinachothibitisha yale yaliyokitangulia; na ameshafunua Torati na Injili kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu, na kwa ajili ya kutofautisha kati ya jema na baya. (Al- Imran 3:2-3) Hapa tunajifunza jambo moja muhimu kwamba kumbe Quran ni Kitabu chenye ukweli. Hapa Allah anachosema ni kuwa, kila kitu Quran inachokisema ni kweli. Ikisema kuwa Wakristo wa kweli ni viumbe bora kuliko viumbe wote duniani, basi, kwa kadiri ya aya hii, hilo ni kweli maana kila ikisemacho ni kweli. Lakini pia, aya hii inatufundisha mambo mengine mawili muhimu, kwamba: 
(i) Kwanza, Quran ipo pia kwa ajili ya kuthibitisha Torati na Injili (Torati ni Agano la Kale na Injili ni Agano Jipya katika Biblia). 
(ii) Torati na Injili zinawaongoza wanadamu (si Wakristo) katika kujua lipi jema na lipi baya. 
Kuna aya kadhaa zingine zinazotudhihirishia kuwa Torati na Injili ni vitabu vya muhimu sana: 
Sura ya Al-Nisa 4:136 inasema: 
O believers, have faith in Allah and His Apostle, in the Book He has revealed to His Apostle, and in the Book He formely revealed. 
Yaani: Enyi mlioamini, iweni na imani kwa Allah na Mtume wake, na kwa Kitabu alichomfunulia Mtume wake, na kwa Kitabu alichokifunua kabla. Tunachojifunza hapa ni kuwa, kumbe tunatakiwa pia kuamini Kitabu kilichotangulia, alichokifunua kabla, yaani Torati na Injili. Na kwa vile tumeona kuwa Quran ni Kitabu chenye ukweli, basi neno hili halina ubishi kabisa. Ni neno la kuaminiwa. Je, wewe unakifahamu kilichoandikwa katika Torati na Injili? Kama sivyo, unaagizwa ukifahamu. 
Sura ya Al- Ahqaf 46:12 nasema: 
Yet before it there was the Book of Musa, a guide and a blessing to all men. This Book confirms it. Yaani: Na bado, kabla yake kulikuwa na Kitabu cha Musa, mwongozo na 
baraka kwa wanadamu wote. Kitabu hiki kinakithibitisha. 
Sura ya Yunus 10:37) inasema: 
This Quran could not have been composed by any but Allah. It confirms what was revealed before it and fully explains what was revealed before it and fully explains the Scriptures. There no doubt about it from the Lord of the creation. Yaani: Quran hii haikuandikwa na yeyote isipokuwa Allah. Inathibitisha kilichofunuliwa kabla yake na inaeleza kwa ukamilifu kilichofunuliwa kabla yake na inaeleza maandiko kwa ukamilifu. Hakuna shaka kuihusu kutoka kwa Bwana wa uumbaji wote. Katika aya hii ya Yunus 10:37, pia tunaambiwa mambo muhimu mawili kuwa: 
(i) Quran inatoa uthibitisho wa kile kilichotanguliayaani Torati na Injili. 
(ii) Quran inachokisema ni kweli na hakina shaka. 
Kwa hiyo, kumbe Quran inatambua kuwa Torati na Injili ni vitabu au maandiko ya muhimu kabisa. Ndiyo maana inasema kwamba: If you are in doubt of what We have revealed to you, ask those who have read the Book before you. Yaani: Endapo mna shaka juu ya yale tuliyowafunulia, waulizeni wale waliosoma Kitabu kabla yenu. (Yunus 10:94). Ni wazi kwamba, Kitabu hapa ni Torati na Injili na waliokisoma ni Wakristo. 
UMUHIMU WA KUWAULIZA WAKRISTO Lakini kwa nini kuwauliza Wakristo? Quran yenyewe isiyokuwa na shaka 
kama inavyojishuhudia, inatupa jibu la kwa nini kuwauliza Wakristo. Inasema: The unbelievers among the People of the Book and the pagans shall burn forever in the fire of Hell. They are the vilest of all the creatures. But those that embrace the faith and do good works are the noblest of all creatures. Yaani: Wale wasioamini miongoni mwa Watu wa Kitabu na wapagani wataungua milele katika moto wa jehanamu. Hao ni waovu kuliko viumbe wote. Lakini wale wanaoikumbatia imani na kutenda mema ni waadilifu kuliko viumbe wote. (Al-Bayyina 98:6-7). Aya hii inaeleza kwamba, miongoni mwa Watu wa Kitabu, yaani watu wanaoamini Biblia, kuna waamini wa kweli na wale wanaojiita Wakristo lakini hawaamini. Ni Wakristo jina tu. 
Basi, hawa Wakristo jina pamoja na wapagani wataingia jehanamu milele. Lakini Quran inasema, Wakristo wa kweli ni viumbe wema kuliko viumbe wote wa Mungu. 
Kwa hiyo, kumbe ni jambo la faida kuwauliza Wakristo wanaokumbatia imani yao sawasawa kwa kuwa ni waadilifu, yaani ni wema na wenye haki. Tena tumeona kuwa Quran inawasema kuwa ni waadilifu kuliko viumbe wote aliowaumba Mungu. Wote!! Sasa ni mtu gani ambaye hangependa kupata kilicho bora kuliko vyote? Wakristo wa kweli ni wale Wakristo ambao Quran inasema kuwa: Among the People of the Book, there are some who, if you trust them with a heap of gold, will return it to you intact, and there are others who, if you trust them with one dinar, will not hand it back unless you demand it with importunity. Yaani: Miongoni mwa Watu wa Kitabu, wapo baadhi ambao ukimkabidhi rundo la dhahabu, atakurudishia likiwa kamili, na kuna wengine ambao, ukimpa dinari moja hakurudishii isipokuwa umemghasi kwa kumdai tena na tena. (Al-Imran 3:75). Hii ni kweli kabisa. Wala hili halina ubishi kwa mtu yeyote anayeipenda kweli. Kwa hiyo, kumbe basi tunaona jinsi ambavyo Quran inawathamini Wakristo walio waaminifu na kuwaambia wanaomwamini Allah kuwa, wawaulize hao pale wanapokuwa na shaka. Kwa maana nyingine pia ni kuwa wanatakiwa wasome Torati na Injili. Katika kuhitimisha sehemu hii ya “Quran Isemavyo Kuhusu Torati na Injili”, tumetambua kuwa, kumbe Quran ambacho ni Kitabu kisicho na shaka, inawaagiza Waamini wake kuwa, wanatakiwa kuamini Torati na Injili kwani inasema: O believers, have faith in Allah and His Apostle, in the Book He has revealed to His Apostle, and in the Book He formerly revealed. Yaani: Enyi mlioamini, iweni na imani kwa Allah, na kwa Kitabu alichomfunulia Mtume wake, na kwa Kitabu alichokifunua kabla. (Al-Nisa 4:136) Na Kitabu alichofunua kabla ni Torati ya Musa na Injili ya Isa/Yesu. 

Itaendelea

4 comments:

  1. Injili. Yoh 10:22-30
    22 Ilikuwa sikukuu ya Utakaso wa Hekalu wakati wa majira ya baridi, 23 na Yesu alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika ukumbi wa Sulemani. 24 Wayahudi wakamzunguka wakamwuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo utuambie wazi wazi.” 25 Yesu akawajibu, “Nimewaambia lakini hamuamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yan anishuhudia. 26 Lakini hamuamini kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu. 27 Kondoo wangu husikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata; 28 nami ninawapa uzima wa milele. Hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka katika mikono yangu. 29 Baba yangu ambaye amenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwatoa hawa kutoka katika mikono yake. 30 Mimi na Baba yangu tu mmoja.”
    anajitambulisha kuwa yu mungu

    ReplyDelete
  2. kuhusu yesu kuwa mwana wa mungu mkuu
    Luka 1:30-33 BHND
    Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema. Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu. Yeye atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
    na ndio maana mungu ni mmoja katika nafsi tatu
    yaani mungu baba, mwana na roho mtakatifu. hakuna awezae kukiri hayo kama asipoongozwa na roho wa mungu.

    hakuna alietoka kwa mungu kwaajiri ya wokovu zaidi ya Yesu Kristu wa nazareth ambaye yeye ndie atakae kuja kwaajiri ya kuuhukumu ulimwengu.

    na kama Quran ya mkiri yesu kuwa ni masiha kwanini haimfuati na kumwamini kama yeye ndie njia ya ukweli na uzima hakuna aweae kumwona baba bila kupitia kwa njia ya mimi. Rejea injili ya Yohane 14:6 maneno yaYesu Mwenyewe kama waiamini Quran na Quran yamkiri yesu kuwa ni Masiha basi jua njia ya kwenda mbinguni ni Yesu Kristu ambae mungu ameliweka jina lake kuwa kuu kupita majina yote. Amini in Islam but Jesus is the way to heaven.

    ReplyDelete
    Replies

    1. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake. Kwa hivyo atautawala ukoo wa....
      Swali ??? Mfalme Daudi ni mwana 😃😃😃

      Delete
  3. Uwongo mtupu msitapetape ovyo

    ReplyDelete