Kwanza kabisa basi, naomba dua, sala, maombi na sala za shukrani zitolewe kwa Mungu kwa ajili ya watu wote. Kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema. Jambo hili ni jema na lampendeza Mungu Mwokozi wetu. 1 Timotheo 2:1-3
Kama tunavyoona katika maandiko haya, tunafaa kuomba kila aina ya maombi tukijiombea na kuwaombea wengine pia. Hebu tuangalie aina tofauti ya maombi ambayo inafaa kuomba tunapoanza kujifunza kuomba kwa moyo bila kukoma. Ombi la kujitolea umkabidhi BWANA njia yako, pia umtumaini, naye atafanya. Zaburi 37:5.
Kwanza kuna maombi ya kujitolea
Hapa tunayatoa maisha yetu na kumkabidhi Bwana. Tunafanya hivyo tunapompa hofu zetu. Kama tunavyoambiwa katika 1 Petro 5:7 “…Mwekeeni matatizo yenu yote, maana yeye anawatunzeni.”
Wakati tunapokumbwa na hofu ya mambo na shida ambazo zinatishia kutuangamiza, tunahitaji kuomba: “Bwana, mimi sitaubeba mzigo huu wa matatizo na kuukubali unitese na kunizuia kukutumikia. Baba ninaomba sasa hivi kwamba utanipa nguvu na kuniwezesha kufanya yale ambayo umeniitia kufanya hata kama nitayafanya nikiwa mwenye hofu. Ninakuwekea shida hii, chochote kiovu, kibaya au cha kuchukiza, ambacho shetani anajaribu kunionyesha kwamba kitanitokea. Ni shauri lako, si langu kwa maana nitafanya yale uliyoniambia na nikuachie hayo mengine.” Iwapo tutaomba mara tu hofu inapojitokeza— basi tutaona hofu hiyo ikishindwa kwa nguvu za Mungu.
Shida ni kwamba, si hofu kubwa ambazo hututatiza sana. Mara nyingi ni hofu ndogondogo ambazo hutuandama usiku na mchana ndizo hutuibia uzima na furaha yetu kama vile mbweha wadogo ambao huharibu mizabibu (Wimbo 2:15).
Ndio maana, unapohisi hofu, hata iwe ndogo kiasi gani, unahitaji kuomba, “Bwana, sitaishi kwa hofu. Badala yake, ninakukabidhi maisha yangu na ninakuomba ushindi juu ya jambo hili ambalo linajaribu kunitesa na kunizuia kuishi maisha kamili ambayo unatamani niishi na kutimiza mpango wako mzuri na mkamilifu.” Iwapo tutaomba hivyo kwa moyo na dhati, basi Bwana ataheshimu maombi yetu na kujitoa kwetu na atatimiza sehemu yake ya kutuweka huru. Maombi ya Kujitakasa au Kujiweka Wakfu Kwa hiyo, ndugu zangu, maadam Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: jitoleeni nafsi zenu kwa Mungu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza.
Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu. Warumi 12:1 Wakati tunapokitoa kitu kwa Mungu katika maombi, hilo huwa ombi la kuweka wakfu. Tunapofanya hivyo tunasema, “Bwana, ninakupatia pesa zangu, wakati wangu, nia yangu”— chochote kile tunachomtolea Bwana.
Mtume Paulo anatuhimiza katika maandiko haya tutoe, na kuweka wakfu miili yetu kwa Bwana, viungo vyote vya miili yetu vipate kumtumikia, ambayo ndio njia yetu halisi ya kumwabudu. Sisi pia huomba ombi la kuweka wakfu wakati tunapowatoa watoto wetu kwa Bwana, tukiahidi “…kuwalea katika kumcha na kumheshimu Mwenyezi—Mungu.” (Waefeso 6:4).
Jinsi tunavyoweka wakfu maisha yetu, pesa na mali yetu, nia na miili yetu, jamii na watoto wetu kwa Mungu, ndivyo pia tunafaa kutoa na kuiweka wakfu midomo yetu—na kufanya hivi kunatuongoza katika aina ifuatayo ya maombi.
Maombi ya Sifa na Ibada
Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa na midomo inayoliungama jina lake. Waebrania 13:15 Nafikiri sote tunafahamu sifa na ibada. Sifa ni kuyarudia mema ambayo Mungu amefanya. Ni kusema hadithi ya mema aliyotufanyia.
Ibada ni kumsujudu. Ni kutambua “Kustahili” kwake. Ni kumtambua Yeye na utukufu wake. Hii ndio sababu mwandishi wa kitabu cha Waebrania anatuambia kwamba inafaa tumsifu na kumwabudu Mungu kila wakati.
Kama tulivyoona, ombi la sifa na ibada linatakiwa kuwa kama kupumua, mchana na usiku, kila wakati. Tunatakiwa kuwa na shukrani kwa Mungu kila wakati. Tukitambua, tukikiri na kulitukuza Jina lake katika maombi, sifa na ibada.
Maombi ya Shukrani
Na muwe na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu. 1 Wathesalonike 5:18 Mara tu baada ya kutuambia katika 1 Wathesalonike 5:17 tuombe bila ya kukoma, Mtume Paulo anatuelekeza tumshukuru Mungu katika kila jambo.
Haijalishi kinachoendelea katika maisha yetu kwa maana hili ndilo kusudi la Mungu kwa ajili ya maisha yetu. Jinsi maombi yanavyopaswa kuwa mtindo wa maisha yetu, ndivyo shukrani inapaswa kuwa sehemu ya maisha yetu. Kumshukuru Mungu hakupaswi kuwa jambo ambalo tunafanya mara moja kwa siku tunapoketi chini na kujaribu kufikiri mambo yote mema ambayo Mungu ametufanyia, na kusema kwa udhaifu, “Asante Bwana.” Hiyo ni dini, jambo ambalo tunafanya kwa sababu tunafikiri kuwa Mungu anatuhitaji tumfanyie. Shukrani ya kweli huendelea kububujika kutoka kwenye moyo ambao umejaa shukrani na sifa kwa Mungu kwa sababu ya utukufu wake na matendo yake.
Si jambo tunalofanya ili atutimizie hitaji fulani, tupate kibali, tupate ushindi, au ili tuhitimu kuweza kupata baraka. Aina ya shukrani ambayo Mungu Baba anatamani kutoka kwetu ni ile ambayo imechochewa na Roho Mtakatifu ndani yetu ambaye anatuvuta tumweleze Bwana yale tunayohisi katika roho zetu. Shukrani ya kweli ni ile iliyoelezwa na mwandishi wa Zaburi aliposema: “Mshukuruni Bwana wa mabwana, kwa maana huruma zake na fadhili zake zadumu milele—” (Zaburi 136:3)!
Maombi katika Roho
Lakini ninyi, wapenzi wangu, endeleeni kujijenga kikamilifu katika imani yenu takatifu. Salini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Yuda 20 Tulikuwa tayari tumeona katika waefeso 6:18 kwamba haitoshi kuomba maombi ya kila aina bila kukoma tu, bali jinsi tunavyoambiwa na Yuda, maombi yetu yanafaa kuwa “katika Roho Mtakatifu.”
Ni Roho Mtakatifu wa Mungu ndani yetu ambaye hutuchochea na kutuongoza kuomba. Badala ya kusubiri, mimi na wewe tunahitaji kujifunza kujitoa kwa Roho Mtakatifu mara tu tunapohisi mwongozo wake. Hii ni sehemu ya kujifunza kuomba kila aina ya maombi kila wakati, popote tulipo, hata tunapokuwa tukifanya chochote. Mwito wetu unafaa kuwa ule wa tenzi ya kitambo iliyosema, “Kila nitakapohisi Roho Mtakatifu akinichochea moyoni, nitaomba.” Iwapo tunajua tunaweza kuomba wakati wowote, mahali popote, basi hatutahisi tunalazimika kungoja hadi wakati na mahali maalum ili tuweze kuomba.
Maombi ya Kukubaliana
Tena nawaambieni, wawili miongoni mwenu wakikubaliana hapa duniani kuhusu jambo lolote la kuomba, Baba yangu wa mbinguni atawafanyia jambo hilo. Kwa maana popote pale wanapokusanyika wawili au watatu kwa jina langu, mimi nipo hapo kati yao.”
Mathayo 18:19,20 Kuna nguvu katika kukubaliana. Biblia inatuambia kwamba iwapo Bwana yu pamoja nao, mtu mmoja anaweza kuwapiga elfu moja, na wawili wanaweza kuwapiga elfu kumi. (Kumbukumbu 32:30).
Lakini nguvu hii inapatikana tu wakati tunakuwa katika makubaliano na wenzetu—pamoja na Bwana. Ni wazi kwamba hatuwezi kugombana na wenzetu kila wakati na kisha tukubaliane katika maombi kuhusu hitaji fulani na tutarajie kwamba “Ombi la kukubaliana” litakuwa na nguvu – ndivyo tunavyoonywa katika 1 Petro 3:7 (UNION):
“Kadhalika nyinyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.” Vivyo hivyo, hatuwezi kunung’unika na kumsengenya mhubiri wa neno wiki nzima na kisha tumwendee kwa maombi kuhusu shida fulani ambayo imetukumba na tutarajie kwamba ataomba ombi la makubaliano pamoja nasi. Kwa nini? Kwa sababu tayari hatumo katika makubaliano na wenzetu na Mungu. Unajua ni kwa nini Mungu anaheshimu maombi ya kukubaliana? Ni kwa sababu anajua kuwa si jambo rahisi kwetu kutembea na kuishi katika makubaliano na wengine. Mungu anamheshimu mtu yeyote ambaye amejitoa kufanya hivyo. Mimi na wewe tukikubaliana na wenzetu na Mungu pia, basi maombi yetu yatakuwa yenye nguvu na uwezo zaidi. Maombi ya pamoja “Hawa wote walikusanyika pamoja kusali…”
Matendo 1:14 Kuna nguvu kubwa katika maombi ya pamoja, ambayo ni aina mojawapo ya ombi la kukubaliana kama inavyodhihirika katika mstari huu tuliosoma. Katika kitabu cha Matendo, tunasoma kwamba watu wa Mungu walikuja, “wakakusanyika pamoja” (Matendo 2:1, 46, 4:24, 5:12, 15:25). Katika Wafilipi 2:2, tunaambiwa na mtume Paulo, “Ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia, moja, kusudi moja, na upendo mmoja.”
Iwapo tutayafuata maneno haya na tuishi na kukubaliana na wenzetu na Mwenyezi Mungu, tutaona matokeo ya ajabu kama walivyoona wafuasi wa kwanza katika kitabu cha Matendo.
Maombi ya Maombezi
Kwanza kabisa, basi naomba dua, sala, maombi na sala za shukrani zitolewe kwa Mungu kwa ajili ya watu wote. 1 Timotheo 2:1 Kumfanyia mtu maombezi, ni “Kusimama pengoni kwa ajili yake.” Ni kumwombea mbele ya kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu.
Katika Warumi 8:26,27, tunaambiwa na mtume Paulo kwamba Roho Mtakatifu hutuombea kulingana na mapenzi ya Mungu.
Katika Waebrania 7:25 tunasoma kwamba Yesu “…anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu.” Mwishowe, Paulo anatuhimiza hapa katika 1 Timotheo 2:1, tuwafanyie maombezi watu wote. Kumaanisha kwamba tunatakiwa kuwaombea watu wote kila mahali.
Maombezi ni mojawapo ya njia muhimu kabisa katika kuendeleza huduma ya Yesu aliyoianzisha hapa duniani.
Maombi ya Kukaa Kimya
…Bwana yu hekaluni Mwake; dunia yote na iwe kimya mbele zake. Habakuki 2:20
Mimi huita aina hii ya maombi, “kumngojea Bwana.” Daudi alijua kuhusu kumngoja Bwana kama tunavyoona katika Zaburi 27:4 alipoandika:
“Jambo moja ninalitamani, kwamba nikae nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa Bwana na kutafakari katika hekalu mwake takatifu.” Ni muhimu sana kujifunza kumngoja Bwana kwa sababu watu wengi hawaelewi kwamba ni muhimu kufanya hivyo katika maombi. Maombi si jambo tunalofanya tu, bali pia ni kuwa na nia ya kungoja. Maombi si kumzungumzia Mungu kila wakati—ni kumsikiza pia.
Maombi ya Mahitaji Binafsi
Msifadhaike juu ya jambo lolote; lakini katika kila jambo mjulisheni Mungu haja zenu, kwa kusali na kuomba pamoja na kushukuru. Wafilipi 4:6 Ombi la kibinafsi ni kumwomba Mungu akutane na mahitaji yetu. Mimi husema kwamba ombi kuu kabisa ambalo mtu yeyote anaweza kuomba ni ombi ninaloliita, “Ombi la Nisaidie”. “Mungu nisaidie, nisaidie, Ee Mungu nisaidie!”
Mimi huliomba sana. Wakati mwingine mimi huamka usiku wa manane kwenda kujisaidia, na sina shida yoyote; bali ninajikuta ninaomba, “Ee Mungu, nisaidie, nisaidie mimi!” Ninaamini ni Roho Mtakatifu aniongozaye kuomba hivyo. Ombi hili la “Mungu nisaidie” ni ombi lenye nguvu sana. Iwapo mimi na wewe tumefika mahali ambapo hakuna la ziada tuloweza kufanya, tunaweza kuomba hivi. Ombi lingine la kibinafsi ni lile ninaloliita, “Bwana, Nakuhitaji.”
Tunaweza kuona mabadiliko makubwa katika maisha yetu iwapo tutaacha kujaribu kufanya kila kitu kwa nguvu zetu wenyewe. Mithali 3:5-7 inatuambia: “Mtegemee Bwana kwa moyo wako wote, naye anainyosha njia yako. Usiwe mwerevu machoni pako, bali mche na kumwabudu Bwana na kuachana na maovu.” Usingoje mpaka wakati utakapokuwa umeshindwa na kutambua kwamba huwezi kushinda peke yako ndipo umkimbilie Mungu akusaidie.
Tambua kabla hata hujajaribu, kwamba huwezi lolote kwa nguvu zako. Mtegemee Mungu kabisa. Jifunze kuomba hivi: “Bwana, siwezi kufanya jambo hili, lakini wewe unaweza kwa kunitumia mimi. Ninakutegemea na kukutazamia, nikiwa na tumaini ndani yako kwa moyo wangu wote. Nisaidie Bwana, kwa maana ninakuhitaji.” Ombi hilo dogo linatosha kukuwezesha kushinda hali mbaya mno maishani. Kutambua kuwa Mungu ndiye msaada wetu huchukua muda mfupi sana lakini kunaweza kutusaidia kushinda kushindwa katika hali za maisha yetu ya kila siku—hasa tunapogundua kwamba bila Bwana hatuwezi chochote. Unaposema, “Bwana, ninakutegemea, nisaidie tafadhali,” umeomba ombi la kibinafsi—nalo lina nguvu. Haya ndiyo maombi tunayotakiwa kuomba tunapowasilisha hitaji la aina yoyote.
Tumia kanuni hii: jiambie; “Jinsi ninavyoendelea kuwa na shughuli nyingi, ndivyo ninavyohitaji kutumia muda mwingi na Bwana.” Kwa sababu jinsi nilivyo na mengi ya kufanya, ndivyo ninavyohitaji msaada zaidi kutoka kwake. Ukiwa mtu wa shughuli shughuli kama Martha kiasi cha kwamba huna wakati wa kukaa na Bwana, basi wewe una shughuli kupita kiasi. Unahitaji kuwa kama Maria na ujifunze kuachana na mambo mengine yasiyo ya maana sana ili upate kukaa miguuni pa Bwana na kujifunza kutoka kwake. Ukifanya hivyo, basi utapata funguo za ufalme kutoka kwake!
No comments:
Post a Comment