Sunday, 27 May 2018

NEEMA INAKUJA SIKU YA LEO.


“Kuwaza na kuwazua” hutuweka katika mtego wa mambo ya kale au hujaribu kutusukuma tuishi katika siku za usoni. Kumbuka Biblia inasema, “Imani  Sasa  ni…” (Waebrania 11:1).  Ukijaribu kuishi maisha ya kale, itakuwa vigumu mno.  Mungu hakujiita “Mungu Mkuu Aliyekuwa.”  Ukijishughulisha na mambo kuhusu jinsi ya kuishi maisha ya kesho au ukijaribu kutambua kila jambo litakalotendeka, maisha yatakuwa magumu.  Hakujiita “Mungu Mkuu  Atakayekuwa.”  


Lakini ukiishi siku moja hadi nyingine, siku ya leo, siku uliyo nayo leo, maisha yatarahisishwa kabisa.   Alisema, “Mimi Ndiye” (Kutoka 3:14).  Imani Sasa   ni… Aliwaambia wanafunzi wake katika mawimbi na upepo mkali baharini, “Mbona mwaogopa? Jipeni moyo.  Mimi Ndiye!”. (Mathayo 14:27, maneno ya ziada ya mwandishi.)  Unayaelewa haya?   Yesu alikuwa akisema “Mimi Ndiye” niliye hapa kwa ajili yako sasa, na “Mimi Nikiwepo,” kila jambo litakuwa sawa.  Ishi katika siku ya leo!  Wasiwasi kuhusu jana au kesho hutuibia siku ya leo.  Umepewa neema ya leo.  

Neema ya kesho haitakuja hadi kesho itakapofika, na neema yote ya jana imetumika. Neema ni uwezo, fadhili na nguvu za Roho Mtakatifu zinazotupa msaada wa kutenda chochote tunachohitaji kufanya.  Lakini hatupati neema awali ili tuirundike kwenye stoo. Je, unakumbuka wana wa Israeli jangwani?  Mungu aliwalisha kila siku kwa njia ya muujiza kwa kuwanyeshea chakula chao kutoka mbinguni. Walikiita “manna.”  Kama ilivyo sisi, walitaka kuhakikisha kuwa walikuwa na chakula cha kutosha cha leo na kesho pia.  Walitaka  kuhakikisha kwamba kesho imeshugulikiwa ikiwa Mungu angesahau kutenda muujiza wake asubuhi iliyofuata.  Lakini Mungu alikuwa amewapa onyo wasikusanye chakula cha ziada katika siku moja, ila tu siku kabla ya Sabato.  Na walipokusanya chakula cha ziada katika siku moja, chakula hicho kilioza.  
Tia tamati hapa na utafakari mambo haya.  Huu ni mfano wenye nguvu ambao tunaweza kuutumia maishani mwetu leo. Je, ukiwaza na kuwazua, ukiwa na wasiwasi na mikereketo, si hiyo inaonyesha kuwa unajaribu kuweka “manna” ya kesho kwenye stoo?  Baba yako wa mbinguni anataka umwamini kuhusu mambo ya kesho.  

Mithali 3:5 (AMP) inasema tumwamini Bwana kwa mioyo yetu na nia (mawazo) zetu zote, na tusitegemee maarifa yetu. Wakati mmoja nilisoma kielezo hiki:   Wanaume wawili walifungwa jela kwa sababu ya ushuhuda wao kumhusu Yesu Kristo.   Walitakiwa kuuwawa kwa kuchomwa moto asubuhi ya siku iliyofuata.  Mmoja wao alikuwa ni mzee aliyekomaa katika njia za Mungu na yule mwenzake alikuwa kijana chipukizi aliyempenda Bwana sana, lakini hakuwa na uzoefu katika njia za Mungu. Kijana huyu aliwasha kiberiti ili awashe mshumaa usiku ulipokaribia. Alipokuwa akiwasha mshumaa, alichoma kidole chake. Kisha akaanza kukasirishwa na kupiga mayowe kwa woga akisema, “Lo! ikiwa kuchomwa kidole kunaumiza hivi, nitawezaje kuvumilia kuchomwa moto mwili wangu wote?   Yule mzee alimfariji kwa maneno haya, “Mwanangu, Mungu hakuagiza ujichome kidole, ndio maana hakukupa neema.   Anakuhitaji tu utoe maisha yako yawe kama kafara, na unaweza kuwa na uhakika kuwa kesho ikifika utapata neema ya kutenda unachohitaji kufanya.”  

Unajua, yule mzee,  aliyekuwa na uzoefu mwingi katika njia za Mungu alifahamu, kwa sababu ya kutembea na Bwana miaka mingi kuwa bila shaka asubuhi iliyofuata, neema ingekuwepo. Kwa hivyo alitulizwa moyo leo  kwa sababu alikuwa anaishi katika imani  leo, maana kesho uwezo (neema) ungekuwepo. Unaweza kuona kutoka kwenye mfano huu kwamba imani inatuweka huru tokana na “kuwaza na kuwazua.”  Imani haina lazima ya kutatua shida za siku za usoni. Imani hupumzisha maana inajua Mungu atanyesha manna ya kesho. 

Ninakutia moyo usiharibu siku ya leo kwa kujaribu kutatua (kuwaza na kuwazua) yaliyopita au yajayo. Wakati mmoja nilisoma usemi huu: Siku ya jana ni kama cheki ya benki iliyofutwa; kesho ni kama barua ya ahadi ya kupata pesa na leo tu ndio pesa taslimu ulizo nazo sasa.   Itumie siku ya leo kwa busara.

No comments:

Post a Comment