...bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya. Watapanda juu kwa mbawa kama tai... Isaya 40:31 (SUV)
Mara kwa mara watu huhisi kuwa mtu akitarajia zaidi ya alivyo navyo basi ni mlafi au anafanya makosa. Ijapokuwa ni kweli kwamba wakati wote tunapaswa kuridhika na kutosheka na yale tuliyo nayo, haimaanishi kuwa kutamani kuwa na vitu vizuri ni makosa alimradi tuna sababu nzuri ya kuvitamani. Tunawezaje kutosheka na huku bado tunataka kuwa na vingi? Mimi sasa hivi ninatosheka sana na kila kitu katika maisha yangu kwa sababu ninaamini wakati wa Mungu maishani mwangu ndio mzuri zaidi. Ninaweza kufurahi hata kama sina kitu chochote cha ziada kwa sababu furaha yangu na kutosheka kwangu viko katika Kristo. Hata hivyo, wakati huo huo ninataka niwe na vitu vingi zaidi kwa sababu ninataka niendelee katika maisha kadri Mungu atakavyoniruhusu na nimfanyie mengi na pia niwafanyie wengine mengi iwezekanavyo. Sitaki kitu kingine zaidi isipokuwa maisha mazuri zaidi ambayo Mungu anataka kunipa! Ninamtaka Mungu zaidi maishani mwangu, ninataka kuwa karibu naye, niishi ndani yake (Wafi lipi 3:10). Ninataka hekima zaidi, uthabiti zaidi, na marafiki wengine zaidi walio wazuri.
Ninataka wanangu wawe na kila kitu, na ninataka watu wengine zaidi wampokee Yesu kuwa Mwokozi wao. Ninataka kuona miujiza mingi zaidi, watu wakiponywa zaidi, ushindi, na nguvu.
Ninaamini kabisa kwamba tunaweza kutosheka kufikia kiwango cha kutosumbuka au kutokuwa na wasiwasi na yale tuliyo nayo, na wakati huo huo tukitamani mengi zaidi kwa sababu fulani nzuri na kwa wakati ufaao (Wafilipi 4:11. 19). Kusema kweli ninaamini kwamba wale wanaotosheka na kiwango cha chini cha yote ambayo Mungu anaweza kuwatendea wanazuia ukuu wa Mungu. Anataka ajidhihirishe kuwa ana nguvu katika maisha ya kila mmoja wetu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu (Waefeso 3:20).
Pandisha Kiwango Chako cha Matarajio
Umtumainie BWANA, uwe imara, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA. Zaburi 27:14 “Matarajio makubwa ndio ufunguo wa kila kitu.” —Sam Walton
Hebu niwasimulie kisa cha mwanamke mmoja aitwaye Betty. Betty ni mwamini. Yeye husoma Biblia mara kwa mara. Mara moja kwa mwezi yeye hujitolea kwa kuwagawia blanketi watu wasiokuwa na makazi. Betty anaonekana mtu mzuri, sivyo? Mm, kuna kitu fulani kuhusu Betty ambacho sharti ukijue: Anapokuwa hayupo marafiki zake humwita “Betty-Yule Mbaya” Wanahisi vibaya juu ya jina hilo alilobandikwa, lakini pasipo kumwonea, Betty alijitafutia jina hilo; ana namna ya kutarajia, kutabiri, na kutafuta yale mabaya zaidi katika kila hali. Nitawapa mfano. Majira ya kiangazi yaliyopita, Betty na mumewe (Phil Ambaye Hufanikiwa) walienda likizoni pamoja na watoto wao wawili (Will Ambaye Hatafaulu Vile na Pack Megan Aliye Katikati). Sasa, lazima niwaambie kwamba Phil ni mume mzuri anayempenda mkewe na Will na Megan ni watoto wazuri sana, lakini Betty hana matumaini makubwa juu yao. Hatarajii mambo mengi kutoka kwao pia. Kusema kweli, kwa kiasi fulani anatazamia mabaya, sawa na majina waliyobandikwa..
Miezi kadhaa iliyotangulia, Phil na Betty walipanga kusafiri na kwenda likizo ya wiki nzima mahali mashuhuri kwa ajili ya mapumziko, lakini safari ilipokaribia, Betty alifahamu fika kwamba mambo hayatakwenda vizuri. Walipokuwa njiani wakiendesha gari umbali wa maili 300 kuelekea mahali pa likizo, Betty muda wote alikuwa akilalamika na kusema, “Wazo la kwenda likizo halikuwa zuri.” Sehemu za kufanyia chochote katika bustani zitakuwa na foleni ndefu ya maili moja. Siamini ikiwa hoteli tutakayolala itakuwa nzuri kama ilivyotangazwa. Mvua itanyesha wiki nzima.” Phil na watoto walijaribu kumhakikishia Betty kwamba kila kitu kitakwenda vizuri—wanaweza kutumia vizuri hali yoyote itakayotokea—lakini hali ya Betty ya kuona kila kitu kuwa giza haikuweza kuondoka. Maskini Phil, Will, na Megan ...waliuona mwendo huo wa maili 300- kwa gari ukiwa kama maili 1,000 za kuchosha sana. Kwa kweli mambo yalikwenda sawa na matarajio ya Betty.
Foleni za bustani ya maji zilikuwa ndefu kuliko kawaida. Phil, Will, na Megan hawakujali—hali hii iliwapa muda zaidi wa kucheka pamoja na kupanga watakuwa kwenye msafara wa ngapi—lakini Betty alikuwa amekasirika sana.
Alinong’ona na kusema, “Nilijua tu haya yangetokea.” Ule mkahawa waliochagua kwenda kula chakula cha jioni usiku ule wa kwanza vile vile haukuwa mzuri. Mhudumu wa kike alimweleza Phil na Betty kwamba vinywaji laini walivyokuwa wameagiza vilikuwa vimeisha. Phil aliagiza kinywaji kingine; Betty yeye akachagua kununa tu. Akaguna na kusema, “Ajabu hii!” Lakini kitu kilichowaudhi zaidi ni kile walichokiona walipoingia katika chumba chao cha hoteli. Walipoingia chumbani mwao ili walale, waligundua kwamba TV ilikuwa haifanyi kazi vizuri. Betty alilalamika tena na kusema, “Nilijua tu!” Nilijua! Nilijua! “Nilijua hii hoteli si nzuri kamwe.” Phil aliwaita wahudumu wa sehemu ya mapokezi, na mafundi wakaja mara moja na televisheni mpya, lakini tayari mambo yalikuwa yameharibika. Betty Mbaya alikuwa na likizo mbaya...hivyo ndivyo alivyotarajia haswa.
Swala la Moyo Kisa cha Betty ni cha kubuni tu na kinahusu mtu ambaye kwa kiasi fulani anafanana na mimi na wewe wakati mwingine. Tumejikuta tukipambana na hali ya kutoona mafanikio na kutokuwa na matarajio makubwa—tukiiona hali ya hewa kuwa “ya mawingu kiasi” badala ya kuiona kuwa yenye “jua kiasi,” tukiiona glasi ikiwa “tupu nusu” badala ya kuiona “imejaa nusu.” Kwa Betty, matarajio yake madogo yalimzuia kufurahia likizo yake ya wakati wa kiangazi, lakini kwa watu wengi, matarajio madogo huwazuia kufurahia maisha yao. Wanaishi kila siku huku wakiwa na mitazamo hasi, ya kutafuta makosa, kukosoa kila kitu, na ni nadra sana kwao kutarajia mema kwa sababu wanajishughulisha sana kutarajia mabaya zaidi. Wakati mambo hayaendi vizuri wanajisemea Nilihisi leo itakuwa siku mbaya, mambo yanapokwenda vizuri wanasema Yamkini hii haitadumu kwa muda mrefu. Siku iwe njema au mbaya, wawe juu mlimani au bondeni, hawafurahii maisha yao... kwa sababu hawakutarajia watayafurahia. Huenda mimi na wewe si wabaya kama Betty, lakini kusema kweli, kiwango chochote cha kukosa matumaini kina athari kubwa maishani mwetu. Kwa nini wasiamini mema na wafungue mlango waone mambo ambayo Mungu anaweza kuwafanyia? Matarajio madogo ni zaidi ya malalamiko kidogo ya siku ndefu ya Jumatatu au kuhisi pengine umeamka vibaya. Matarajio madogo ni dalili ya tatizo kubwa zaidi, tatizo la kiroho. Mtu anaweza kuwa na historia ya kuvunjwa moyo iliyomfanya awe na mazoea ya kutarajia mambo kama hayo zaidi kila wakati. Watu wengine wana kiwango cha chini cha kujistahi kiasi kwamba wanajiona kuwa hawafai kuwa na kitu chochote kizuri, hivyo hawatarajii chochote.
Na kisha kuna wale watu wengine ambao hawajui Mungu ni mwema na anataka kuwatendea mema wanawe. Hatari zinazotokana na dalili hizi kubwa. Kama tungeeleza yale yanayoendelea katika nafsi zetu kama ambavyo tunaeleza ugonjwa wa mwili, basi ingekuwa kama hivi:
Daktari: Kwa hiyo, unasema husikii vizuri kiroho na kimwili. Tafadhali niambie dalili za ugonjwa wako.
Mgonjwa: Mmm, Daktari, ninahisi vibaya kuhusu siku za usoni. Nimevunjwa moyo mara nyingi maishani mwangu, na sitarajii ikiwa mambo yataniendea vizuri au hata familia yangu.
Daktari: Dalili zako zinaniambia kila kitu ninachopaswa kujua. Una tatizo kubwa la ukosefu wa matumaini.
Dalili za Betty zilikuwa kuona kila kitu ni kibaya, wasiwasi, na kulalamika. Dalili hizi zilisababishwa na tatizo la moyo wake: ukosefu wa matumaini. Badala ya kutarajia likizo nzuri ya familia, Betty alitarajia mambo mabaya sana. Foleni zitakuwa ndefu.
Hatutapata mkahawa mzuri. Hoteli itakuwa mbaya sana. Hakuna matumaini yoyote katika mawazo kama hayo. Hata hivyo, Phil, Will, na Megan walionyesha dalili tofauti. Walikuwa na mtazamo chanya, walisisimka, wakafurahi, na walikuwa tayari kukabiliana vizuri na hali yoyote. Walijaa matumaini, na matarajio yao yalikuwa ya juu sana. Ni muhimu kutambua kwamba mazingira yalikuwa yale yale kwa Betty na familia yake, lakini jinsi walivyoyapokea mazingira hayo ni tofauti. Wote walisimama kwenye foleni ndefu; wote walikula kwenye mkahawa mmoja; wote walikaa chini mbele ya televisheni iliyoharibika. Mambo haya yalipotokea, matarajio madogo ya Betty yalithibitishwa, hali iliyomfanya atake kukata tamaa.
Kwa wengine katika familia hiyo, matarajio yao makubwa yalikumbwa na changamoto, lakini wakachagua kuendelea kuwa na matumaini na furaha, jambo lililowawezesha kupata njia za kukabiliana na mazingira hayo na kusonga mbele, huku wakifurahia kila hatua ya mwendo wao. Basi ukiwa na taswira hiyo, ningependa nikuulize swali muhimu: Dalili zako ni zipi? Kama ungeuchunguza vizuri moyo wako, je, ungeona nini ndani yako? Je, wewe ni kama Phil, Will, na Megan? Waliosisimshwa na mambo yaliyokuwa mbele yao, wakitarajia leo iwe siku nzuri zaidi kushinda jana na kesho iwe siku nzuri zaidi kuliko leo?
Je, huwa unaamka kila asubuhi ukiwa na furaha na matarajio kwamba Mungu anaenda kutenda kitu cha ajabu mashani mwako? Au wewe ni kama Betty Mbaya? Je, huwa unajikuta unajiandaa kukabiliana na mambo mabaya? Je, huwa una wasiwasi wa mambo mabaya kutokea hata kabla hayajatokea? Je, huwa unatumia maneno kama ndiyo haya tena, hili halitafaulu kamwe, natamani ningejua kwamba mambo yatatumbukia nyongo, na ninahisi vibaya juu ya jambo hili? Je, huwa unaamka kila asubuhi ukiwa na furaha na matarajio kwamba Mungu anaenda kutenda kitu cha ajabu maishani mwako? Kuunganika kwa Imani Kuitathmini mioyo yetu ni shughuli muhimu wakati tunapoanza safari hii ya matumaini pamoja, kwa sababu kumtumaini Mungu na kuwa na matarajio mazuri yana uhusiano wa karibu sana na imani. Kwa sababu ya majadiliano, tunaweza kusema kwa urahisi kwamba kiwango cha matarajio yako ndicho kiwango cha imani yako. Nionyeshe mtu mwenye matarajio madogo, nami nitakuonuyesha mtu anayetumia imani haba. Lakini nionyeshe mtu mwenye matarajio makubwa, na nitakuonyesha mtu anayetumia imani ya kijasiri. Kumbuka tunaongea kuhusu kuwa na matarajio yetu katika Mungu. Hilo ni zaidi ya kuwa na mtazamo chanya; ni kumtegemea Mungu akutunze na atunze kila kitu kinachokuhusu wewe. Neno la Mungu linatwambia kwamba imani yetu— matarajio yetu chanya, yenye matumaini—humpendeza Mungu (Waebrania 11:6), na mara kadhaa katika Injili, tunamuona Yesu akichochewa kutenda jambo kwa sababu ya imani—na matarajio— ya wale aliokutana nao (Mathayo 9:29, Marko 5:34, Luka 7:50 na Luka 17:19). Mmoja wa miujiza kama hiyo unapatikana katika Marko sura ya 10. Ninaipenda hadithi hii, na nafikiri ina umuhimu mkubwa kwako na kwangu leo kwa sababu inahusu umuhimu wa matarajio. Marko 10: 46–47 inasema: ...
[Yesu] alipokuwa akiondoka kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu.
Unapofikiria juu ya tukio hilo, utaona kwamba Bartimayo alikuwa na sababu za kutosha za kutarajia mabaya zaidi. Alikuwa ni kipofu mwombaji aliyekaa kando ya njia kila siku, akijaribu kuwaomba watu wampe pesa.
Alikuwa anaishi maisha magumu sana, na ikiwa kuna mtu ambaye angeshusha chini matarajio yake, basi angekuwa ni Bartimayo. Angefikiria na kusema Hii haina maana yoyote. Haiwezi kufaulu. Hakuna kitu kitakachobadilika. Yamkini Yesu hata hataniona. Kwa nini niwe na matumaini? Hakuna mtu ambaye angemlaumu. Lakini Bartimayo alithubutu kutarajia kitu kizuri zaidi katika maisha. Alianza kufikiria juu ya kile ambacho huenda kingetokea badala ya kufikiria kile ambacho huenda kisingetokea. Hakuna kitu “kilichoshushwa chini” kuhusu kiwango chake cha matarajio wakati alipoanza kupaza sauti kwa nguvu zake zote, “Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu!
Je, unaweza kusikia msisitizo huo katika sauti yake? Ni kana kwamba Bartimayo alikuwa ameamua kwa vyovyote hatakosa fursa hii. Ijapokuwa wengi waliokuwa katika kundi lile la watu “walimkemea ili anyamaze” (Marko 10:48), Bartimayo hakukubali kunyamazishwa. Alipaza sauti zaidi na zaidi hadi Yesu akasimama na kumwita. Hii hapa ni moja ya sehemu za ajabu za hadithi hii: Bartimayo alipoletwa kwa Yesu, Bwana alimuuliza swali ambalo huwezi hata kudhani angeulizwa. Katika kifungu cha 51, Yesu alimuuliza yule kipofu mwombaji, “Wataka nikufanyie nini?” Hilo linaonekana kuwa swali la ajabu, sivyo? Huenda wanafunzi walikuwa wanajisemea “Wataka nikufanyie nini?” Bwana, si ni wazi kabisa? Huyu bwana ni kipofu. Unawezaje kumuuliza swali kama hilo? Lakini Yesu alikuwa anauliza swali la kina zaidi—Alikuwa anamuuliza Bartimayo: Unatarajia nini? Je, unatarajia chakula? Je, unataka akushike mkono na kukuelekeza? Je, unatarajia kupewa kitu? Mambo hayo yote bila shaka yalikuwa mambo ambayo Bartimayo alihitaji, na kama angekuwa na imani haba, angetosheka na kimoja cha vitu hivyo. Lakini Bartimayo alikuwa na kiwango cha juu cha matarajio. Yesu alipomuuliza, “Wataka nikufanyie nini?” Bartimayo hakusita, hakuwa na haja ya kuanza kufikiria juu ya jambo hilo, hakushangaa endapo anaomba zaidi ya ipasavyo. Bartimayo alisema kwa ujasiri, “Mwalimu wangu, nataka nipate kuona.” Yamkini unajua sehemu ya hadithi hii iliyobaki. Yesu aliguswa sana na imani ya Bartimayo. Kifungu cha 52 kinasema: “Yesu akamwambia, Nenda zako, imani yako imekuponya.
Mara akapata kuona; Akamfuata njiani.” Kwa kuwa Bartimayo alikuwa jasiri kuamini kwamba atapokea mema zaidi kutoka kwa Mungu, hivyo ndivyo haswa alivyopokea kutoka kwa Bwana. Hivyo ndivyo ilivyo hata katika maisha yako, na hivyo kiwango chako cha matarajio ni muhimu sana kwa aina ya maisha utakayoishi. Ikiwa hutarajii Mungu atende jambo lolote kubwa maishani mwako, basi hatatenda. Lakini ukithubutu kupandisha kiwango chako cha matarajio na kuanza kutarajia kwamba Mungu anataka kutenda kitu kizuri katika maisha yako, utaanza kuwa na ndoto, amini, omba, na utende kwa ujasiri uhodari, huku ukijua Mungu yuko upande wako na ana mpango mzuri kwa maisha yako. Kama unauliza ikiwa inakubalika kwa wewe kutarajia mambo mazuri kutoka kwa Mungu, tafadhali soma pole pole na utafakari Maandiko haya katika Isaya.
Kwa ajili ya hayo BWANA atangoja [kwa bidii], [akitarajia, akitazamia na akitamani] ili awaonee huruma, na kwa ajili ya hayo atatukuzwa, ili awarehemu. Kwa maana BWANA ni Mungu wa hukumu. Heri (wana furaha, wana bahati, wanaweza kuonewa wivu) wote wamngojao [kwa bidii], wanaotarajia na kutazamia na kumtamani [kwa ushindi wake, kibali chake, upendo wake, amani yake, furaha yake, na uwepo wake usio na kifani, na usioweza kuharibibwa]! Isaya 30:18 Mungu anawatafuta wale ambao anaweza kuwatendea mema, na ikiwa unamtafuta (unamtarajia) Mungu akutendee mema, basi unafaa. Mtarajie Mungu ajitoe kwako kwa sababu yeye ni muhimu kuliko kitu chochote kile, lakini kumbuka yeye ndiye mwenye mambo mengine yote tunayohitaji. Hatua Tatu Za Kuinua Kiwango Cha Matarajio Yako Huenda unasoma sura hii na kufikiria Joyce, hayo unayosema ni mazuri sana, lakini ninapaswa kutarajia mengi zaidi kwa njia gani? Ninaharakisha kuhudhuria mkutano mmoja hadi mwingine, naona vigumu kulipa madeni yangu, najaribu kuwalisha watoto au kuendesha kampuni ili isifilisike. Maisha yangu yote nimekuwa nikifanya kazi kwa bidii kadri ya uwezo wangu kufikia hapa nilipo.
Ninawezaje kuongeza kiwango changu cha matarajio? Ninaweza kusema mengi sana juu ya imani—maelfu na maelfu ya vitabu vimeandikwa juu ya mada hii—lakini ningependa kukupatia hatua tatu rahisi zinazoweza kukuwezesha kuanza leo. Hatua hizi tatu zitakusaidia kupandisha kiwango chako cha matarajio:
1. Amini. Kuna sababu inayofanya wana wa Mungu waitwe “waamini.” Unapojaribiwa kuwa na mashaka, unapojaribiwa kukata tamaa, unapojaribiwa kufa moyo, chagua kuamini. Kuamini ndio msingi wa imani yako.
Amini. Neno la Mungu. Amini kwamba ahadi zake, ni za kweli. Amini anakupenda, na amini ana kitu kizuri kwa ajili ya maisha yako. Yesu alisema Unapojaribiwa kuwa na mashaka, unapojaribiwa kukata tamaa unapojaribiwa kufa moyo, chagua kuamini. ikiwa tungeamini tu, basi tungeona utukufu wa Mungu (Yohana 11:40). Utukufu ndio dhihirisho la uzuri wote wa Mungu.
2. Omba. Yakobo 4:2 inasema: “Hamna kitu kwa kuwa hamwombi.” Utakapochagua kuamini kuwa Mungu anaweza kukimu kila hitaji maishani mwako, basi endelea mbele na umwombe Mungu akimu mahitaji hayo. Mshirikishe ndoto zako. Kama vile Yesu alivyomuuliza Bartimayo, “Wataka nikufanyie nini?” Anakuuliza swali hilo hilo. Kuwa na ujasiri wa kumwomba Bwana afanye kitu ambacho yeye peke yake ndiye anayeweza kukifanya. Bila shaka, sote tunapaswa kutaka Mungu atende mapenzi yake na tuamini kwamba ikiwa kile tunachomwomba si kitu kizuri kwetu, basi Mungu hatatupatia lakini badala yake atatupatia kitu kizuri zaidi.
3. Tazama. Unapoishi kila siku, tarajia kwamba Mungu anajibu maombi yako, anakimu mahitaji yako, na kutimiza ndoto aliyokupa Mungu. Hata ikiwa bado hujaona dhihirisho la yale unayotamani, au ikiwa hayajatokea kama ulivyotarajia, hiyo haimaanishi kwamba Mungu hafanyi kazi. Endelea kuwa na mtazamo wa matarajio, na uhakikishe unatambua kila kitu anachofanya Mungu. Shukuru kwa ajili ya mambo hayo huku ukisubiri kitu unachotamani au kuhitaji sasa hivi. Chochote unachokitarajia leo—kuwa karibu zaidi na Mungu, kulielewa Neno la Mungu vizuri zaidi, kuwa na ndoa nzuri, kufanikiwa kifedha, fursa ya kuongeza kiwango cha elimu, nafasi ya huduma, mwanzo mpya—ikiwa yako moyoni mwako (na ikiwa yanaendana na Neno la Mungu), amini, omba, tarajia, na tazama.
Imeandaliwa na Mtumishi Jimmy J.
No comments:
Post a Comment