Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda mengi… Yakobo 5:16
Wakati mmoja, Bwana alinizungumzia maneno haya; “Omba kuhusu kila kitu, na usiogope chochote.” Aliniambia hivi nilipokuwa na hofu kwamba kinyozi wa nywele ambaye nilikuwa nimemwendea kwa mara ya kwanza hangeweza kutengeneza nywele zangu vizuri.
Roho Mtakatifu alinizungumzia, “Usiogope hali hii. Wewe iombee. Omba kwamba Bwana atampa upako kinyozi huyu ili aweze kufanya kile kinachohitajika.”
Kisha katika majuma yaliyofuatia, Bwana aliendelea kunionyesha mambo tofauti kuhusu vile maombi yanavyoishinda hofu.
Mengi yao yalikuwa ni maeneo madogo madogo ambayo hofu hujaribu kuingia na kuniletea shida. Alinionyesha kuwa katika kila hali, haijalishi ukubwa au udogo wake, suluhisho la hali hiyo lilikuwa ni maombi.
Usiogope, kwa maana ni pamoja nawe; usiangalie huku kule kwa hofu na kutahayarika, kwa maana mimi ni Mungu wako. Nitakupa nguvu wakati wa magumu, nitakusaidia. Nitakuinua kwa mkono wangu wa kuume… Isaya 41:10,13 Katika maandiko haya, Bwana anawaambia watu wake wasiangalie huku na huko wakiwa na hofu au wasiwasi, kwa maana yeye ni Mungu wao. Wakati mwingine sisi huogopa tunapoangalia hali ambayo tumo ndani yake. Haya ni makosa. Jinsi tunavyoendelea kukaza macho yetu na midomo yetu kwenye shida, ndivyo tunavyoendelea kushikwa na hofu. Badala yake, tunafaa kuweka macho yetu na midomo yetu juu yake Mwenyezi Mungu.
Yeye anaweza kutatua lolote ambalo litatujia katika maisha haya. Mungu ameahidi kutupatia nguvu, na kutuimarisha katika magumu, kutuinua na mkono wake wa kuume. Anatuamrisha pia tusiwe na hofu.
Lakini kumbuka, yeye hatuamrishi tusihisi hofu au woga, bali tusikubali hofu au woga ututawale. Mungu anatuambia mimi na wewe, “Usiogope, nitakusaidia.” Lakini hatuwezi kuupokea msaada wa Mungu mpaka tutakapojiachilia na tuwe watiifu na kutenda atuambialo kwa imani. Je, unajua ni wakati gani ninahisi upako wa kuhubiri? Ni wakati ninapopanda jukwaani nianze kuhubiri—si kabla ya kuanza. Mungu anatuambia leo, “Acha kukubalia hofu itawale maisha yako.” Anza kufanya yale ninayokuambia ufanye, kwa maana ninayokuambia ni kwa faida yako mwenyewe.
Ninajua baraka zilizo ng’ambo ya pili, lakini ibilisi pia anazijua. Hii ndio sababu anakupinga kwa kutumia hofu na ndio sababu mimi ninakuambia usiogope.
” Usiogope, Wewe Ni Wangu! …
Hivyo asema Bwana, aliyekuumba, Ee Israeli, aliyekutengeneza Ee Yakobo; usiogope kwa maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe ni wangu. Utakapopita kwenye maji, nitakuwa nawe; utakapopitia mito, haitakugharikisha. Utakapopita kwenye moto, hutachomeka, na miali ya moto haitakuunguza. Isaya 43:1-2.
Bwana anatuambia hapa tusiogope wakati tunapopitia majaribu ya kila aina. Hii inamaanisha kwamba tutapata ushindi katika maisha yetu, lakini itakuwa ni wakati tunapopitia mambo hayo. Kuweza kupitia mambo hayo, ni lazima tuamue kwamba hatutakimbia mbele ya majaribu tena. Bwana ameahidi kuwa nasi na kutuweka salama wakati tunapopitia maji mengi ambayo hayatatugharikisha na tunapopitia moto ambao hutatuunguza au kutuchoma.
Je, unaikumbuka hadithi ya wale vijana watatu wa Kiebrania walioitwa Shadraka, Meshaki na Abednego? Walitupwa katika tanuru ya moto mkali lakini hawakuumia kabisa. Hawakuwa hata na harufu ya moto. (Danieli 3:1-30).
Kuna hofu za kutisha, kama ya kutupwa katika tanuru la moto— na kuna hofu ndogo ndogo, kama kuogopa kwamba nywele zako hazitatengezwa vizuri! Unaweza kuwa unaogopa kitu kikubwa kama vile kansa au mshtuko wa moyo au kifo cha mpendwa katika jamii. Au unaweza kuwa unaogopa kitu kidogo kama mvua wakati wa matembezi au kukosa mahali pa kuegesha gari lako.
Haijalishi chanzo au ukubwa wa hofu yako, ni lazima hofu hiyo itatuliwe kwa njia ile ile. Kama tulivyoona, ni lazima ikabiliwe kwa maombi na neno la Mungu. Na wakati tunapoomba, ni lazima tuamini. Hofu ni adui yetu na tunatakuwa kuichukulia kuwa adui.
No comments:
Post a Comment