Saturday, 30 June 2018

Je,Kuhusu Mimi...?

Kwa sasa  hivi, huenda  unafikiria,  na je, kuhusu  mimi?  Ni  nani atakayenifanyia  jambo mimi?  Hili  ndilo  jambo ambalo kwa  kawaida hutuzuia sisi  kuishi  maisha ambayo Mungu  anapenda tuishi. Inanirudia “mimi”  kila mara. Je, kuhusu mimi, kuhusu mimi?     Tumezoea  kuona kwamba matarajio yetu yametimizwa,  kwamba wazo  la  kujisahau  sisi  wenyewe hata  siku  moja  ni  la kutisha. Lakini, ikiwa  tunaweza  kuwa  na ujasiri mkuu wa  kujaribu, tutashangazwa na uhuru  na furaha tutakayopata. Kwa  maisha  yangu mengi, mimi  huamka  kila siku  na kujilaza kitandani  nikifanya mipango yangu. 
Nilifikiri  juu  ya kile nilichotaka  na kitakachokuwa  bora kwangu na jinsi  ninavyoweza kuishawishi familia yangu  na marafiki washirikiane nami katika mipango yangu. Niliamka na kumaliza siku  nzima nikiwaza  akilini mwangu, na kila wakati mambo yalipokuwa hayaendi  nilivyotaka, nilikasirika, nilishindwa  kuvumilia,  nilitatizika na kukasirika sana. Nilifikiri  sina raha  kwa  sababu sikuwa nikipata  kile  nilichotaka, lakini  nilikosa furaha  kwa sababu  yote nilikuwa  nikijaribu  ni  kupata kile nilichotaka bila kuwajali wengine. Kwa vile sasa nimegundua kuwa siri ya furaha ni katika kuyatoa maisha yangu kuliko kujaribu kuyahifadhi mimi mwenyewe, asubuhi zangu  huwa  tofauti.
Asubuhi hii, kabla   nianze kazi  ya  kuandika ukurasa  huu, niliomba na  kisha  nikachukua  muda  wa  kufikiria watu wote ninaojua kuwa  tutawasiliana  nao leo. Kisha nikaomba kupitia Warumi  12:1, “basi, ndugu  zangu,  nawasihi  kwa  huruma zake Mungu, itoeni miili yenu  iwe dhabihu iliyo hai,  takatifu, ya kumpendekeza  Mungu, ndiyo  ibada  yenu yenye maana.”  Neno linaloongea  kuhusu  kujitolea  kwetu kwa  Mungu kama  dhabihu zilizo hai, tutoe uwezo wetu wote wa  hali na mali kwake Mola kwa matumizi  Yake.  Nilipokuwa  nikifikiri  kuhusu watu nitakaofanya kazi nao ua pengine  kuwaona  siku  ya leo, nilimuuliza  Bwana anionyeshe kitu chochote  ambacho  ninaweza  kuwafanyia.  Niliweka wazo  akilini  mwangu niwahimize na niwapongeze. Kwa  kweli  sote twaweza  kupata  kitu kizuri cha  kumwambia  mtu tunayekutana naye. Kujaribu kufanya hivi  kutatusaidia kuondoa akili zetu kwenye mawazo  ya  kujifikiria  sisi binafsi. Ninaamini Bwana  ataniongoza ninapofanya  kazi  yangu  ya  siku ya  leo.

Ikiwa  unataka  kujitoa kwa  Mungu ili  akutumie  kuwapenda na kuwasaidia  wengine, ninapendekeza  uombe  ombi hili.  “Bwana,  Ninakupa macho  yangu, masikio, mdomo, mikono, miguu, moyo, pesa, zawadi, vipawa, uwezo, wakati, na nguvu zangu.  Nitumie  mimi  ewe Bwana,  niwe baraka kila mahali niendako siku ya leo.”
Huwezi kujua furaha  ya kuishi  kama  hivi  hadi pale utakapojaribu. Ninaiita  “tabia  takatifu,”  na  kama  tabia  zote  lazima
itekelezwe kwa vitendo ili iweze kuwa tabia. Siku  nyingine  huwa  ninashikwa na mambo yangu mengi  na husahau  kutekeleza  tabia  yangu  mpya,  lakini ninakumbushwa haraka  wakati ninapopoteza  furaha  yangu   na  tabasamu  ya  maisha kwamba kwa mara nyingine nimetoka nje ya mkondo. Nimekuwa nikijaribu kuishi  namna hii kwa  miaka  kadhaa,  na yamekuwa ni mapambano. Maisha  ya “ubinafsi”  yamekita mizizi katika nafsi zetu na hayafi  kwa  urahisi. Nimesoma vitabu kuhusu upendo,  na  kusoma  tena na  tena   kile Biblia inachosema  kuuhusu na  kuomba  kuhusu jambo  hili. Nimezungumza  na  marafiki  kuuhusu, kuhubiri  kuuhusu, na  kufanya  yote  niwezayo  kuuhifadhi katika  mawazo yangu.  Wakati mwingine  ninapotambua kwamba nimekuwa  mchoyo tena, sikasiriki  kwa sababu kujikasirikia kutanifanya nizidi  kuwa mimi  tu. Ninaposhindwa,  Namuuliza Mungu anisamehe na  nianze upya;  na ninaamini hiyo ndiyo sera bora ifaayo.
Tunapoteza muda  mwingi kuhisi  vibaya kujihusu kwa makosa tunayofanya na hiyo ni  kupoteza wakati. 

Ni  Mungu pekee  anayeweza  kutusamehe  na yuko tayari kufanya hivyo ikiwa tutamuuliza. Ndio,  ninaamini kuwa  chanzo  cha  tatizo  ulimwenguni ni uchoyo, lakini inawezekana uishi  katika uliwengu huu  na ukatae kuwa  kama  ulimwengu ulivyo. Ikiwa  utaungana  nami katika kuanza  mageuzi ya  upendo,  ikiwa utabadilika kabisa  katika  jinsi ulivyokuwa  ukiishi na  uanze kuishi kwa  kupenda kuliko  kupendwa, basi unaweza  kuwa  sehemu ya  suluhisho  kuliko sehemu  ya  tatizo. Je, uko tayari kuanza?

No comments:

Post a Comment