Watu wasiokuwa na lakufanya huvunjika moyo kwa urahisi, hulemewa kimawazo, na kujisikitikia wenyewe. Wanaweza kuanguka katika aina zote za dhambi. Mtume Paulo hata alisema ikiwa mwanamke aliye bado kijana amekuwa mjane, anapaswa kuolewa tena. Lau sivyo huenda asiwe na lakufanya na kuanza masengenyo na kuwa mdakuzi wa mambo (angalia Timotheo 1 5:11-15). Paulo aliendelea kusema kwamba baadhi ya wajane ambao bado wangali vijana kwa kutokuwa na lakufanya tayari walikuwa wameanza kumgeukia shetani. Ina umuhimu gani kuendelea kuwa imara? Ninaamini maandiko ya Paulo yanathibitisha kwamba ni muhimu.
Kwanza, katika maandiko Mungu anatuhimiza sisi tusiwe watu wa kutokuwa na lakufanya. Nyakati za Agano la Kale, wakati mtu alipofariki wana wa Israeli waliruhusiwa kuomboleza mpendwa wao kwa siku thelathini (angalia KUM 34:8). Kwanza, huenda ikaonekana kuwa si muhimu, lakini Mungu alifanya sheria hiyo kwa sababu alijua kwamba muda mrefu wa kuomboleza na kutokuwa na lakufanya unaweza kusababisha matatizo mabaya. Lazima tukae imara tusijihusishe kupita kiasi bali tujihusishe vyakutosha ili tuweze kuendelea katika mwelekeo ufaao.
Kujipanga katika mambo tunayoyafanya ni muhimu. Hatuwezi kutumia muda wetu wote kusaidia watu wengine, lakini kwa upande mwingine, kutotumia muda huo kulingana na mpango huenda kukasababisha matatizo. Ikiwa unaweza kumkumbuka mtu unayemjua asiyekuwa na lakufanya, na ambaye hajishughulishi na jambo lolote pengine pia utatambua kwamba hawana furaha kwa sababu kutojishughulisha na jambo lolote na kukosa furaha mambo haya mawili huwa pamoja.
Miaka kadhaa iliyopita shangazi yangu alihitaji kuhamia katika makazi ya kupewa usaidizi. Kwa miaka mitatu au minne ya kwanza alitaka kukaa tu bila kufanya lolote. Alihuzunika kwa vile aliondoka nyumbani na hakuwa na nia ya kushiriki katika maisha mapya yaliyokuweko. Ingawa kulikuwa na shughuli nyingi na hata nafasi za kusaidia wengine, hakutaka kufanya lolote. Siku baada ya siku alikaa tu nyumbani kwake na alivunjika moyo. Alihisi vibaya mwilini na mara nyingine alikuwa na wakati mgumu kukabiliana na hali hii. Hatimaye alifanya uamuzi kwamba hangeendelea kukaa tu bila kufanya lolote na akajihusisha na mafunzo ya Biblia na kutembelea wagonjwa katika hospitali iliyo karibu na makazi yake. Alicheza michezo, akahudhuria karamu, kukutana na marafiki wengi. Muda si muda alikuwa akinieleza kuwa ana furaha zaidi kuliko alivyokuwa maishani mwake na anahisi vizuri zaidi mwilini.
Hali ya mtu mlegevu huanza kuwa mbaya hadi mbaya zaidi hadi ulegevu wake unapoanza kuathiri kila sehemu ya maisha yake. Yeye huruhusu kuyumbushwa huku na huko na mazingira yake na hali ilivyo. Huwacha hisia zake zimuongoze, na kwavile hajihisi kufanya lolote, yeye hutazama tu na kulalamika huku maisha yake yakisambaratika. Anataka kufanya mambo mengi, ilhali amezongwa na hisia asizoweza kuzieleza. Anahisi ulegevu na hana mawazo ya ubunifu. Anaweza hata kuanza kufikiria kuwa kuna kitu kilicho kasoro mwilini mwake na hiyo ndiyo sababu hana nguvu. Kwake yeye, maisha yamekuwa urithi wa matatizo mengi. Kujiruhusu kukaa tu bila kufanya lolote mara nyingi hutokea baada ya kupata pigo au msururu wa mambo ya kughadhabisha, au wakati mikasa inapotokea, ambayo nitazungumzia mwisho wa mlango huu. Wakati mambo kama haya yanapotokea, huenda tukataka kukata tamaa, lakini tunapofanya hivyo, shetani anasubiri kuingia na kuchukua fursa ya hali ilivyo. Hatuwezi kwa sababu yoyote kuruhusu ulegevu kumpa nafasi adui aingie katika maisha yetu.
No comments:
Post a Comment