Mtumaini Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe.Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako. Mithali 3:5-6 Baada ya mtu kupatwa na msiba au pigo fulani, karibu kila mmoja wetu hupitia hali ya kuomboleza. Kwa kawaida, kuna viwango saba katika kuomboleza. Hebu tuvichunguze viwango hivi kwa makini na tujaribu kupata ufahamu ni nini kinachokuwa kikitendeka katika nafsi zetu na kile tunachoweza kufanya ili kupitia kiwangi hicho kitufaidi kikamilifu.
Kiwango Cha 1: Kushtuka na Kukataa Mara nyingi, mambo haya mawili huwa ndiyo ya mwanzo kutokea tunapopatwa na pigo au msiba. Mungu huyatumia kutulinda ili tusivunjike kabisa. Kushituka: Mshituko ni hali ambayo inagutusha nia na hisia zetu kwa pigo kubwa mno ambalo halikutarajiwa. Kuweza kushtuka ni hali tunayozaliwa nayo ndani yetu. Hutupatia muda wa kuweza kukubaliana na mabadiliko yaliyotukia. Hutuzuia kukumbana na ukweli mara moja.
Kabla yetu kusonga mbele, ni lazima tuwe tumepata nia mpya. Kushituka hutupatia muda wa kujenga upya nia zetu kuhusu maisha yetu ya sasa na ya baadaye. Kwa mfano.
Fikiria Shock Absorbers* za motokaa.Zimetengenezwa ili kuituliza gari wakati inapopitia barabara yenye mashimo. Bila yake, basi gari linaweza kuvunjika vipande kutokana na mapigo inayopata inapoenda huku na kule. Mara nyingi, sisi huwa hivi pia. Tunasafiri katika barabara ya maisha, na wengi wetu hawatarajii mashimo na barabara mbovu. Hivyo tunakuwa hatujajitayarisha wakati mashimo yanapotokea. Shock absorbers zetu ambazo zimewekwa na Roho Mtakatifu hutuliza pigo lile hadi tunapokuwa na uwezo wa kubadilisha nia na mawazo yetu kuweza kukubali na kukabili mabadiliko ya ghafla yaliyoingia katika maisha yetu. Kipindi cha mshutuko kinaweza kudumu kutoka dakika chache hadi wiki kadhaa. Lakini kikipita muda huo, basi kuna shida fulani. Mshutuko ni kama dawa za kuzuia uchungu wakati wa kufanyiwa upasuaji. Lakini hatuwezi kuendelea kuzitumia dawa hizo daima. Ni lazima tuendelee na maisha. Kushituka ni kuepuka ukweli kwa muda, lakini iwapo si kwa muda mfupi, basi huenda kukaleta madhara mengi zaidi. Ninakumbuka nilikuwa na shangazi yangu wakati mjomba alipoaga dunia.
Alikuwa ameugua kwa muda, na ingawa ilikuwa wazi kwamba hangeishi sana, shangazi yangu aliendelea kusema tena na tena, “Siwezi kuamini. Siwezi kuamini ameenda.” Alikuwa katika kiwango cha kwanza cha kushtuka ambacho kwa kawaida huja baada ya msiba. Wakati ambapo unapopitia kipindi cha kushituka, ni vyema usikae bila ya kufanya chochote kwa muda mrefu sana.
Wakati unapopitia kushituka kwa sababu ya msiba fulani, wewe kama mkristo, unahitaji kutofautisha kati ya nafsi yako, na roho yako. Hata wakati wa msiba, unahitaji kupambanua tofauti kati ya hisia zako na mwongozo wa kweli wa Roho Mtakatifu.
Kukana: Kukana ni kuukataa ukweli wa mambo na kunaweza kutuletea magonjwa ya hisia na nia katika vipimo mbali mbali. Mungu ametupatia Roho wake ili tuweze kuupokea ukweli kwa ujasiri, tumshike mkono, na kutembea kati kati ya mabonde yote ya giza na kushinda vizuizi vyote tunavyopitia maishani. Huku tukiwa na Roho wa Mungu ndani yetu kutulinda, tunaweza kusema pamoja na mfalme Daudi, “Ndio, hata nijapopita kwenye bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa lolote. Maana wewe Mwenyezi Mungu u pamoja nami. Gongo lako na fimbo yako vyanilinda.
Hata wakati mauti yanapoleta uvuli wake juu yetu, tunaweza kuishi na tumaini.Tunapozungumza juu ya tumaini, fikiria tena kuhusu Shedraki,
Meshaki na Abednego katika tanuru ya moto. (Danieli 3:8-27). Hata ingawa walitupwa ndani ya tanuru iliyotiwa moto mara saba zaidi, Bwana alikuwa pamoja nao katika moto huo.
Tunaweza kusoma hadithi za Biblia kama hii ambayo tumetaja hapo juu wakati tunapojikuta katika hali ngumu. Kama vile Mungu alivyokuwa pamoja na watoto wale wayahudi katika tanuru ya moto, hata wakatoka wakiwa wazima bila ya kuumizwa, hivyo ndivyo atakavyokuwa nasi katika kila hali tutakayopitia maishani. Ni mapenzi yake Mungu kwetu sisi kuukubali ukweli wa mambo, tuyapitie na tupate kushinda katika kila njia. Kukumbana na ukweli kunaweza kuwa kugumu, lakini kuukimbia huleta hali ngumu zaidi.
Kiwango Cha 2: Hasira Kiwango cha pili huashiriwa na hasira: hasira dhidi ya Mungu, dhidi ya shetani, dhidi yetu wenyewe, na hasira dhidi ya mtu aliyesababisha uchungu au msiba ule, hata kama mtu huyo, katika kuisababisha hali hiyo alikufa. Hasira dhidi ya Mungu: Kila mtu huamini kuwa Mungu ni mwema, na kwamba anatawala maisha yetu. Hivyo, wakati msiba au pigo fulani linapotokea katika maisha yetu, hatuelewi ni kwa nini Mungu hakuzuia mambo mabaya kama hayo yasitokee na kutuumiza. Kila tunapokutana na pigo baya au msiba, mara nyingi, sisi hukasirika na kuuliza, “Iwapo Mungu ni mwema, na mwenye nguvu zote, kwa nini anakubalia mambo mabaya yawatokee watu wema?” Swali hili hututatiza zaidi hasa iwapo ni sisi, watoto wa Mungu, ambao tunaumia na kuteseka.
Katika nyakati kama hizi, nia zetu na mawazo yetu hutaka kupiga mayowe na kusema, “Sielewi hata kidogo!” Tena na tena swali hili, “Kwa nini Mungu, kwa nini?” linawasumbua wale wanaoomboleza katika maisha yao, na wale wapweke na waliokataliwa pia.
Katika 1 Wakorintho 13:12, Mtume Paulo anaeleza kwamba kutakuwa na mambo tusiyoelewa katika maisha haya: Tunachoona sasa ni kama tu sura hafifu katika kioo, lakini hapo baadaye tutaona uso kwa uso. Sasa ninajua kiasi fulani tu, lakini hapo baadaye nitajua yote kikamilifu, kama vile Mungu anavyonijua mimi. Kufikiri kwingi na kujaribu kutatua mambo ambayo hatutaweza kuyaelewa huleta mateso na kuchanganyikiwa lakini katika Mithali 3:5,6 Biblia inatuambia kwamba kumtegemea Bwana kunaleta uhakika na mwelekeo: Mtumaini mwenyezi Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako. Wakati tumo matatani maishani mwetu, tunahitaji mwelekeo. Maandiko haya yanatueleza kuwa kumtegemea Mungu ndio njia ya kupata mwelekeo huo.
Kumtegemea Mungu huhitaji uwe na maswali ambayo hayana majibu katika maisha yako! Ukweli huu ni mgumu kwa wengi wetu kuukubali kwa sababu utu wa mwanadamu hutaka kuelewa kila kitu. Katika Warumi 8:6, tunaambiwa kuwa “…nia ya mwili … ni akili na mawazo bila Roho Mtakatifu…” (AMP) Sisi hutaka mambo yapate kueleweka, lakini Roho Mtakatifu anaweza kutusababisha tuwe na amani hata ingawa tunapitia mambo yasiyoeleweka kabisa. Haijalishi una uchungu wa aina gani kutokana na msiba wako.
Roho Mtakatifu anaweza kukupatia amani, nawe upate kujua kuwa kila kitu kitaenda vyema. Kumkasiria Mungu hakunaa maana kwa sababu yeye pekee ndiye anayeweza kutusaidia. Yeye tu ndiye anayeweza kuleta faraja ya milele na uponyaji ambao unahitajika. Ninakuhimiza uendelee kuamini kuwa Mungu ni mwema na ujue kwamba chochote kilichotendeka hakibadilishi ukweli huu; Mungu ni mwema. Hata kama huelewi kwa nini mambo yanakwenda kama yanavyokwenda, endela kuamini na kukiri kwamba Mungu ni mwema - kwa maana ni kweli! Katika Zaburi 34:8, mtenzi anatuhimiza, “Jaribuni muone Mwenyezi -Mungu alivyo mwema. Heri Mtu anayemkimbilia usalama kwake.” Kisha katika Zaburi 86:5 anasema, “Wewe ee Bwana, U mwema, na mwenye kusamehe; mwingi wa fadhili kwa wote wakuombao.” Mwishowe katika Zaburi 136:1, tunaambiwa, “Mshukuruni mwenyezi Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele.
Mungu ni mwema, lakini shetani anataka tuamini kwamba hatuwezi kumtegemea Mungu na kwamba Yeye hatujali wala kutupenda. Ikiwa una mashaka kuhusu upendo wa Mugu kwakona uaminifu wa ulinzi wake, tafadhali tafakari maneno haya ya Paulo kuhusu swala hili yanayopatikana katika Warumi 8:35-39: Ni nani awezaye kututenga na mapendo ya Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kuuawa? Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha: tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa.” Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda.
Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: wala kifo, wala uhai; wala malaika, au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; Wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu kwetu kwa njia ya Kristo Yesu Bwana wetu.
Usimkasirikie Mungu. Pokea huduma ya Roho Mtakatifu. Yasikize maneno ya Yesu katika maandiko haya: Yesu aliwaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele. “Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja tena kwenu. (John 14:1, 16,18) Farijiwa na maneno haya na umpinge shetani ambaye atakuwa anajaribu kukufanya umwelekezee Mungu hasira yako na usumbufu wako.
Kumkasirikia shetani:
Biblia inasema tunafaa kuchukia uovu (Amosi 5:15), na kwa kuwa shetani ndiye chanzo cha uovu wote, basi kuwa na hasira juu yake ni sawa - iwapo tunaidhihirisha hasira hiyo kwa njia ya kibiblia. Katika waefeso 6:12, tunaelezwa kuwa, “Maana vita vyenu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu wanaomiliki ulimwengu huu wa giza.” Tafsiri moja ya kiingereza inasema, “Tunapigana dhidi ya watawala wa giza, dhidi ya majeshi ya roho za uovu…”
Ni wazi kwamba vita vyetu si dhidi ya Mungu au watu, bali ni dhidi ya adui Shetani.Je tunaweza kuweka hasira zetu kwa njia ifaayo?
No comments:
Post a Comment