Thursday, 26 July 2018

Acha Kuzungumzia Shida Zako

Je,  umewahi  kugundua  kwamba  Yesu  hakuzungumzia  shida zake?  Angeweza  kufanya  hivyo;  Alikabiliana  na  mambo  yale yale  tunayokabiliana  nayo  mimi  na  wewe.  Yesu  alikuwa  na  ratiba iliyojaa  shughuli. 

Yesu  alikumbana  na  watu  wajeuri  na  wanaoudhi. Yesu  alikabiliana  na  hali  ngumu.  Bila  kutaja  kwamba  alifahamu fika  kwamba  atateseka  sana  na  kufa  msalabani  kwa  ajili  ya  dhambi za ulimwengu. Lakini  ukisoma  Injili,  hutamsikia  Yesu  akisema  chochote  cha kukashifu  au kinachoweza  kuitwa kulalamika au kunung’unika. Bila  shaka  alijua  nguvu  za  maneno.  Wakati  wa  mateso  na  kifo chake ulipokaribia,  aliwaambia  wanafunzi wake  kwamba hatakuwa akiongea  nao kwa muda mrefu  kuanzia wakati  huo na kuendelea (Yohan 14:30).  


Kwa nini alisema hivyo? Ilikuwa ni kwa sababu alijua nguvu  ya maneno, na pia alijua jinsi  ilivyo rahisi  kuongea mambo yasiyofaa wakati tunapitia wakati mgumu au wa uchungu.  Alijua kwamba Baba yake alikuwa na mpango wa kumwokoa mwanadamu na kwamba mpango huo ulimtegemea  yeye, na aliazimia kufanya kila alichotakiwa kufanya ili atekeleze  makubaliano aliyokuwa nayo na Mungu, ikiwemo kuongea  maneno ambayo Mungu angetumia, si maneno ambayo ibilisi angetumia.

           Mimi  sitasema  nanyi  maneno  mengi tena,  kwa       maana  anakuja mkuu  wa  ulimwengu  huu,  wala  hana  kitu kwangu. [Hatufanani kwa lololote;  hakuna chochote  ndani yangu kilicho chake, na hana nguvu juu yangu.] Lakini ulimwengu  ujue  ya kuwa nampenda  Baba;  na kama vile Baba  alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.Yohana 14: 30–31

Bila  shaka,  Yesu  alizungumzia  mambo  mengi,  ikiwemo  dhambi. Kuna  wakati  ambapo  Yesu  aliwakemea  Mafarisayo  na  kuwakosoa wanafunzi  wake. 
Unaposoma  Injili,  utaona  kwamba  Yesu  aliongea kuhusu  mambo mengi,  lakini shida zake hazikuwa  miongoni mwa mambo  hayo.  Luka  4:22  inasema  kwamba  watu  “walistaajabia maneno  ya  neema  yaliyotoka  kinywani  mwake.”  Yesu  alikuwa amekuja kutekeleza  kazi fulani,  na hakutaka kuiacha njia kwa kuangazia  matatizo ya  kila  siku  katika  maisha Alisema  kwamba maneno yake ni roho na tena uzima (Yohana 6:63).

Je, wewe  maneno yako ni roho na tena  uzima, au ni ya kimwili (kibinadamu)  na  mauti?  Habari  njema  ni kwamba unaweza kubadilika hivi sasa ikiwa unataka  kufanya  hivyo. Mimi ndiye  mtu wa kwanza  kukiri  kwamba kinywa  ni kiungo  ambacho huwezi kukidhibiti bila  msaada  kutoka  kwa Mungu. Hata  hivyo, tukifanya uamuzi sahihi na kukubaliana na mapenzi ya Mungu katika sehemu hii, bila shaka atatusaidia kufanya mabadiliko mazuri.

Jimmy J.
Mtumishi.

No comments:

Post a Comment