Friday, 27 July 2018

Vifungo vya nafsi

Kutumia  muda mwingi pamoja na mtu au kitu  fulani,  huleta uhusiano wa karibu na mtu au kitu hicho. Kama wanadamu, sisi  ni roho, tuna nafsi, na tunaishi katika mwili. Nafsi inaweza kuelezwa kama nia, hisia na hiari yetu. Tunapojihusisha  na mtu au kitu, sisi  hutumia muda  mrefu kumfikiria,  kuwaza  juu  ya  mtu  au  jambo  hilo  na  kufanya  mipango inyayohusu uhusiano huo. Kwa kawaida, mazungumzo yetu huwa juu ya mambo ambayo tunahusika nayo katika  nia zetu, mapendekezo yetu  na hisia zetu. 

Ukiliwazia jambo hili, utaona jinsi ‘nafsi’  zetu zinavyohusika zaidi na watu au vitu tunavyotumia muda na nguvu zetu  kushughulikia. Iwapo mkono wangu ungelifungwa kwenye mwili wangu na kukaa pale kwa muda  wa  miaka  mingi  bila ya kufanya chochote, basi matokeo yanaweza kuwa ya kutisha. Iwapo ungelifunguliwa mara,  basi ungekuwa umenyauka,  bila nguvu, na tena umelemaa. Singeweza kuutumia mpaka uweze kupata nguvu tena na uwezo wa kufanya kazi. Ingenibidi nitafute njia  mpya za kuufanyisha mazoezi ili misuli ambayo imedhoofika iweze kupata nguvu.
Hivi ndivyo ilivyo kuhusu nafsi zetu. Wakati tunapohusika na mtu, mahali au kitu fulani kwa muda mrefu, nafsi zetu “hufanganishwa” na jambo hilo.

Wakati mtu au kitu kile kinapochukuliwa kutoka kwetu, sisi  huwa katika hali ya kutaka kuendelea na maisha  kana kwamba kingali kupo. Kama mkono ambao ulikuwa umefungwa kwa muda mrefu, hata ingawa umefunguliwa, unaendelea kuhisi kana kwamba ungali umefungwa. Haufanyi kazi vizuri hadi  baaada  ya muda  ambapo  umefanyishwa  mazoezi  ili uweze kurejea hali yake ya kwanza. Hata wakati tunapoamua kuachana na mtu au jambo fulani, nafsi yetu  inaweza kutamani kuendelea kukaa  pale. 

Hisia zetu zina nguvu mno, nazo zinaweza kutuletea dhiki na uchungu mkuu. Ni lazima tugundue kuwa tunaweza kutumia “hiari” yetu kuamua kukubali au kukataa kufanya jambo  fulani. Uamuzi  thabiti wa hiari yetu, unaweza kushinda  hisia mbaya hata zinapokuja kwetu zikiwa na nguvu nyingi. Kuna “vifungo vya nafsi” vibaya, na kuna vingine vizuri. Vifungo vyema  hufikia  hali  ya  usawa  baada  ya  muda.  Lakini  vile  vibaya huhitaji kukabiliwa na kuondolewa. 

Haijalishi unalishughulikia jambo gani sasa hivi, lisipotatuliwa kwa njia inayofaa, huenda likakufunga zaidi, hata kukuletea ulemavu katika sehemu hiyo ya maisha yako. Hata hivyo, Mungu anajua  jinsi  ya kukufungua!   Iwapo umeumia  kutokana na ajali, pengine itabidi ujifundishe kutembea tena.

Ikiwa umempoteza mwenzi  wako katika kifo au kwa sababu ya talaka, inaweza kukubidi ujizoeze kuishi peke yako. Labda itakubidi ujifunze kufanya kazi fulani ambazo ulikuwa umesahau jinsi zinavyofanywa,  au ambazo hujawahi kufanya  hapo mbeleni. Inaweza kukubidi  utafute kazi au ujifunze kupika  na kuwashughulikia  watoto au kuamua mambo ambayo hujayazoea au hata huyafahamu kabisa.
Iwapo umepoteza kazi, inaweza kukubidi ujifunze kuomba kazi au hata kuhama kwenda mji mwingine. Wakati  unapofanya mambo haya yote,  unaweza kuwa bado una uchungu rohoni, lakini unaweza kufarijika unapojua  kuwa unasonga mbele. Kila siku unapiga hatua.
Mungu ameahidi  kuwa pamoja  nawe wakati wa dhiki.

Wakati unapoendelea kumsubiri akukomboe, unaweza kufarijika kwa kutambua kuwa yu pamoja nawe na anaendelea kufanya kazi kwa niaba yako hata ingawa pengine huoni kwa macho  yako yale anayofanya.

Katika Mathayo 28:20, Biblia inasema, “…na hakika mimi  nipo pamoja  nanyi siku zote, hadi mwisho wa dunia…”
Jimmy J.

No comments:

Post a Comment