Siku moja nilisikia hadithi ya mwanamume mmoja aliyepoteza funguo jioni moja. Basi akawa anazitafuta sana, alizitafuta kwa hasira nje pembezoni mwa moja ya barabara, chini ya mlingoti wa taa za barabarani. Mpita njia mmoja aliona jinsi alivyokuwa akizitafuta kwa bidii na akasimama kumsaidia kutafuta funguo hizo.
Baada ya dakika chache za kutafuta kwa bidii, yule mgeni aliyekuwa anamsaidia alimwuliza akasema, “Sasa, hizo funguo umeziangusha wapi haswa? Kama tukijua ni wapi haswa, huenda tukawa na bahati tukaziona.” Bila kusita, yule mwenye funguo zilizopotea alijibu, “Niliziangusha wakati nilipokuwa nyumbani kwangu.” Yule mgeni aliyekuwa anamsaidia akapigwa na bumbuazi kusikia jibu hilo, akasema kwa mshangao, “Ikiwa umeziangusha nyumbani kwako, mbona unazitafuta hapa chini ya mlingoti wa taa?” Yule aliyepoteza funguo akajibu, “Kwa sababu hapa kuna mwangaza zaidi.”
Yamkini unasema Huu ni upuuzi. Kila mtu anajua kwamba si jambo la busara kufanya hivyo. Linaweza kuonekana jambo la kipumbavu kutafuta funguo zilizopotea nyumbani kwako chini ya mlingoti wa taa za barabarani, lakini ninayo sababu ya kuwasimulia hadithi hiyo.
Mara nyingi katika maisha, tunatafuta kitu tunachohitaji, lakini tunakitafuta mahali pasipo sahihi. Kuna wimbo mmoja wa zamani unaosema “looking for love in all the wrong places-Kutafuta mapenzi mahali pasipofaa.” Nadhani wimbo huo unasema ukweli. Lakini pia ninadhani kuwa mara kwa mara huwa tunatafuta matumaini mahali pasipofaa.
Ikiwa kweli tunataka kufurahia maisha, itabidi tufanye mabadiliko ya kimsingi ya pale tunapotafuta matumaini. Sharti Yesu awe chanzo cha matumaini yetu wakati wote. Haijalishi hali zetu ni za aina gani. Hali zetu hazipaswi kuwa ndivyo vitu vinavyochangia kiwango chetu cha furaha. Hata ikiwa tunaishi katika siku mbaya sana, tunaweza kuwa na mtazamo uliojaa kujiamini, furaha, na matumaini ikiwa tutajifunza kuangalia kile tulichosalia nacho, si kile tulichopoteza. Wakati wote angalia kile anachofanya Mungu, si kile unachofikira hafanyi. Natamani mtu angeliniambia ukweli huu mapema maishani mwangu.
Kwa miaka mingi nilikuwa Mkristo wa kuteseka, anayesumbuka, na moja ya sababu hizo ni kwamba nilikuwa wakati wote nafikiria juu ya kile nilichokuwa sina. Nami sikufikiria tu, bali nililalamika juu yake. Ningetumia muda wangu wa kuomba na kumwambia Bwana mambo yote niliyokuwa sina. Mungu, sina pesa za kutosha. Sina talanta ile waliyo nayo wengine.Orodha ya mambo haya ni ndefu. Nilitazama hapa na pale na kufanya hesabu ya kila kitu nisichokuwa nacho. Lakini Bwana alianza kunionyesha kuwa nilikuwa na vingi tu, nilikuwa natazama mahali pasipofaa. Hakuna ushindi katika kuangazia vitu ulivyopoteza au usivyokuwa navyo.
Badala ya kuweka nguvu na juhudi zangu katika kulalamika juu ya vile nilivyopoteza, Bwana alianza kunifundisha kuangazia vile nilivyosalia navyo. Huenda sikuwa na pesa nyingi kiasi cha kuweza kuwenda likizo ya kupendeza sana, lakini angalau nilikuwa na pesa za kulipia madeni yangu ya mwezi huo. Huenda sikuwa na uwezo ule waliokuwa nao watu wengine, lakini nilikuwa mnenaji mzuri, na hatimaye Mungu akaanza kutumia kipawa hicho kuwasaidia watu.
Mambo haya haya yanaweza kuwa yametokea kwako. Haijalishi unapitia mambo gani leo, unaweza kugundua furaha mpya katika maisha. Huenda umepoteza mambo fulani; huenda kuna faida fulani ambazo huna. Lakini badala ya kuangazia kile ulichopoteza, kwa nini usitafute miongoni mwa kile ulichosalia nacho? Unaweza ukashangaa kwa kile utakachokiona.
No comments:
Post a Comment