Kukumbana na mabadiliko makuu maishani ni moja ya mambo magumu zaidi ambayo tumeitwa kuvumilia. Hata kama ni sisi wenyewe tuliochagua kuwa na mabadiliko hayo, haimaanishi ya kuwa mambo hayo yatakuwa rahisi kwetu. Ikiwa mabadiliko haya yanatokana na msiba, kifo au pigo fulani, basi kuhisi kuchanganyikiwa, kupoteza mwelekeo, na hofu ni kawaida. Kwa sababu ghafla mipango yetu ya usoni inaangamia.Safari ya mapumziko, mpango wa kununua nyumba, pesa za malipo ya uzeeni au mipango mingine ya maana sana kwetu ghafla inaangamia. Inachukua muda mrefu kwetu kupata mwelekeo mpya. Katika nyakati kama hizi, maswali mengi huja katika mawazo yetu, mengi yao yanayohitaji majibu papo hapo. Hata jamaa na marafiki wanaweza kuwa wanauliza tena na tena, “Utafanyaje sasa? Utaishi wapi sasa? Utarejea kazini mara moja au utachukua muda kupumzika?” Yote haya ni maswali mema ambayo mwishowe lazima yajibiwe. Iwapo umepatwa na msiba au pigo ambalo limebadilisha maisha yako, unajua unahitaji kufanya uamuzi katika sehemu kadhaa za maisha yako kuhusu siku za usoni.
Lakini unaweza kuwa unajihisi kwamba huko tayari kufanya hivyo! Nyakati kama hizi, huwa umejawa na mawazo mengi ya kutatanisha. Unaweza kufanya uamuzi fulani, kisha ghafula ukabadili nia kuhusu uamuzi huo. Hisia zako zinaanza kukufanyia mzaha; mara unataka hili mara unataka lile. Inakuwa ni vigumu kufanya uamuzi ukiwa katika hali hii kuliko nyakati za kawaida. Mara nyingi wakati umechanganyikiwa na kukosa mwelekeo hivi, hofu hukuvamia pia. Unaweza kuanza kujiuliza maswali kama haya, “Nitafanyaje kuhusu fedha zangu? Ni nani atakayeanza kushughulikia mambo haya ambayo sijazoea kuyashughulikia?” Unapokuwa umebanwa na mambo kama haya, ninakuhimiza uyatafakari maneno haya kutoka kitabu cha Waebrania.
Maneno haya hunipatia faraja na tumaini, nami naamini yatakutia moyo pia: Mungu mwenyewe amesema: “Sitakuacha kamwe, wala sitakutupa.” Waebrania 13:5 Tunapokuwa hatujui cha kufanya au yale ambayo yanatungojea baadaye, ni jambo la kufariji kumjua yule ayajuaye mambo hayo. Katika Zaburi 139:15-17, mtenzi anatuhimiza kuwa Baba yetu wa mbinguni anajua maisha yetu ya kale, ya sasa, na ya baadaye: Umbo langu halikufichika kwako nilipokuwa ninatungwa ndani ya tumbo la mamangu. Wewe uliniona hata kabla sijazaliwa, uliandika kila kitu kitabuni mwako; siku zangu zote ulizipanga, hata kabla ya kuweko ile ya kwanza. Ee Mungu, mawazo yako ni makuu mno; hayawezi kabisa kuhesabika! Mungu ndiye Alfa na Omega, mwanzo na mwisho. Na kwa sababu hii ni kweli, yeye pia ndiye kila kitu kilicho katikati ya Alfa na Omega.
Anajua hali zetu naye atatuongoza na kutuelekeza iwapo tutamtegemea afanye hivyo. Baba yetu wa mbinguni kwa kawaida hutupatia kile tunachohitaji kuweza kuishi siku kwa siku. Neema ya kuishi katika siku moja hutujia siku hiyo inapoanza. Kwa sababu hii, ni vigumu kuyawazia maisha ya baadaye kwa muda mrefu, bila kuhisi woga. Tunapowazia maisha ya baadaye, sisi huhisi ya kwamba hatuwezi kukumbana na shida ambazo zinaambatana na siku hizo.
Lakini hii ni kwa sababu sisi huwa tunazitazama siku hizo bila neema ya Bwana juu yetu. Tunapofikia mahali au siku fulani, tutaikuta neema ya wakati ule mahali pale. Kwa maelfu ya miaka, Zaburi 23 imewahudumia na kuwafariji mamilioni ya watu ambao wamekuwa wapweke na wenye kuomboleza. Wakati wa kuchanganyikiwa, kupoteza mwelekeo na kuwa na hofu nyingi, wewe tumia maandiko haya kama nanga ya nafsi yako: Bwana ndiye Mchungaji wangu, sitapungukiwa kitu, yeye hunilaza katika majani mabichi, huiongoza kwenye maji matulivu. Huirejeza na kuipumzisha nafsi yangu, huniongoza kwenye njia za haki - kwa ajili ya jina lake. Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa, kwa maana u pamoja nami. Fimbo yako na gongo lako huniongoza. Umeniandalia karama machoni pa watesi wangu, umenipaka mafuta kichwani mwangu. Kikombe changu umekijaza mpaka kufurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata mimi, siku zote za maisha yangu nami nitakaa nyumbani mwa Mwenyezi - Mungu milele.
No comments:
Post a Comment